Jun 12, 2021 12:38 UTC
  • Nujabaa ya Iraq: Tuko tayari kuikomboa Miinuko ya Golan ya Syria

Msemaji wa Harakati ya Muqawama ya Iraq ya al-Nujabaa ambayo ni sehemu ya harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi ya nchi hiyo ametangaza utayarifu wa harakati yake kwa ajili ya kuikomboa Miinuko ya Golan ya Syria.

Nasr al-Shammari amesema hayo katika mahojiano na tovuti ya habari ya al-Ahad yenye makao yake Lebanon na kusisitiza kuwa, harakati hiyo ya kupambana na magenge ya kigaidi imejiandaa kikamilifu kuikomboa Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel, na kwamba utawala huo uko katika ncha ya kuporomoka.

Ameashiria namna harakati hiyo ilivyounda Brigedi ya Ukombozi wa Golan mwaka 2017 na kueleleza bayana kuwa, "licha ya harakati ya al-Nujabaa kuwa amilifu katika vita dhidi ya magenge ya kitakfiri nchini Syria, lakini Brigedi hii iliundwa makhsusi kwa ajili ya kupambana na utawala wa Kizayuni, na hilo litasalia kuwa hivyo."

Msemaji wa harakati ya al-Nujabaa ya Iraq amebainisha kuwa, baada ya kambi ya muqawama kupata ushindi mkubwa katika Operesheni ya Panga la Quds huko Gaza hivi karibuni, vita vijavyo vitapenya ndani zaidi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu, katika maeneo yanayozungukwa na Mto Nile na Furati (Euphrates).

Askari na bendera ya Syria katika Miinuko ya Golan

Ikumbukwe kuwa, mwaka 1967, utawala wa Kizayuni wa Israel uliteka karibu kilomita 1200 za ardhi ya Syria katika Milima ya Golan na baada ya kupita muda uliyaingiza maeneo hayo katika ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na kupachikwa jina la Israel.

Jamii ya kimataifa daima inasisitiza kuwa Milima ya Golan ya Syria itaendelea milele kuwa milki ya nchi hiyo ya Kiarabu. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limetoa maazimio kadhaa ya kuthibitisha kuwa utawala wa Kizayuni unaikalia kwa mabavu miinuko hiyo.

Tags