Jun 13, 2021 11:11 UTC
  • Jumuiya ya Maulama wa Yemen yalaani uamuzi wa Saudia wa kuzuia ibada ya Hija kwa mwaka wa pili mfululizo

Jumuiya ya Maulamaa wa Yemen imelaani uamuzi uliochukuliwa na Saudi Arabia wa kuzuia ibada ya Hijja na Umra kwa Waislamu kutoka nje ya nchi hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo.

Taarifa iliyotolewa leo na jumuiya hiyo imesema kuwa, uamuzi wa serikali ya Riyadh wa kuzuia ibada ya Hija kwa mwaka wa pili mfululizo kwa kutumia kisingizio cha maambukizi ya virusi vya corona umechukuliwa kwa shabaha ya kuihudumia Marekani na Israel. 

Taarifa ya Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini Yemen imesema uamuzi huo wa kuzuia ibada ya Hija mwaka huu unaenda sambamba na malengo ya Marekini na Israel na si ajabu kwamba umebuniwa na kupikwa Washington na Tel Aviv.

Jumuiya hiyo imesema kuwa, uamuzi wa Wizara ya Hija na Umra ya Saudia wa kuwazuia Waislamu kutoka nje kwenda nchini humo kutekeleza ibada ya Hija kwa mwaka wa pili mfululizo ni wa kidhalimu na kuongeza kuwa, serikali ya Riyadh imechukua uamuzi huo kwa kiburi kikubwa. 

Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, ibada ya Hija mwaka huu itafanyika kwa kushirikisha raia na wageni wanaoishi nchini humo wasiozidi elfu 60.Ma

Masjiul Haram

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudia imesema mahujaji hao elfu 60 kutoka ndani ya nchi wanalazimika kwanza kupata chanjo ya virusi vya corona kabla ya kushiriki katika ibada ya Hija ya mwaka huu.

Mwaka jana pia Waislamu wasiozidi elfu 10 wa ndani ya Saudia kwenyewe ndio walioruhusiwa kushiriki katika ibada ya Hija ambayo kwa kawaida huhudhuriwa na Waislamu zaidi ya milioni mbili kila mwaka kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.