Jun 14, 2021 09:19 UTC
  • Majibu ya HAMAS kwa matamshi ya kichochezi na ya kujikomba kwa Wazayuni ya waziri wa Imarati

Matamshi ya kichochezi yaliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Hizbullah ya Lebanon na kundi la Ikhwanul Muslim, yamejibiwa na harakati ya HAMAS ya Palestina.

Abdullah bin Zayed Aal Nahyan, waziri wa mambo ya nje wa Imarati ametoa matamshi ya kichochezi akidai kuwa eti anashangazwa na nchi ambazo zinaona tabu kuziingia harakati za HAMAS, Hizbullah na Ikhwanul Muslimn katika orodha ya makundi ya kigaidi sawa kabisa na magenge ya kigaidi na ukufurishaji kama vile Daesh (ISIS) na al Qaida. Vile vile amezilalamikia hata zile nchi zinazohesabu matawi ya kijeshi ya harakati hizo kuwa ni makundi ya kigaidi na kuacha matawi yao ya kisiasa akidai kuwa, harakati zote hizo ni za kigaidi na hakuna tofauti yoyote baina ya matawi yake.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, matamshi hayo yasiyo na mashiko ya waziri wa mambo ya nje wa Imarati yametolewa kutokana na kuongezeka mapenzi ya wananchi hasa Waislamu kwa harakati za HAMAS na Hizbullah ya Lebanon kutokana na ushujaa wao na kujitolea kwao kupigania haki na kupambana na dhulma. Mapenzi ya watu kwa harakati za mapambano ya Kiislamu kama HAMAS na Hizbullah ya lebanon ni makubwa sana, tofauti kabisa na nchi kama Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ambayo tangu mwaka mmoja nyuma imeonesha mabadiliko makubwa katika misimamo yake ya sisa za kigeni na kushirikiana waziwazi na utawala wa kigaidi wa Israel unaofanya jinai kubwa dhidi ya Waislamu.

Imarati haioni kiwewe kuunga mkono jinai hizi za Israel dhidi ya watoto wa Palestina

Mwaka jana  imarati ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiarabu kusaliti waziwazi malengo matukufu ya Palestina kupitia kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel. Miaka 26 nyuma, yaani mwaka 1994, Jordan ilitia saini makubaliano ya kuishi kwa amani na Israel. Baada ya miaka 26, Imarati mwaka jana ilifungua tena mlango kwa nchi za Kiarabu wa kujidhalilisha kwa uwazi zaidi mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Abdullah bin Zayed Aal Nahyan, waziri wa mambo ya nje wa Imarati ndiye aliyekwenda nchini Marekani kutia saini makubaliano ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala katili wa Israel na alidai kuwa, kwa kufanya hivyo atazifungulia mlango nchi nyingine za Kiarabu zitangaze uhusiano wa kawida na utawala pandikizi wa Israel. 

Suala jingine ni kwamba waziri huyo wa mambo ya nje wa Imarati amekuwa akitoa matamshi ya kuchupa mipaka ya kuunga mkono utawala katili wa Israel kiasi kwamba hata nchi za Magharibi, waitifaki wakubwa wa utawala wa Kizayuni hazitoi matamshi kama hayo. Kila waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu anavyotoa matamshi ya kuchupa mipaka ya kuunga mkono hadharani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina anaona haitoshi na sasa amefikia hadi ya kusema bila kiwewe kwamba eti harakati za ukombozi za wananchi kama HAMAS na Hizbullah ya Lebanon ni sawa tu na magenge ya kigaidi kama Daesh yaani ISIS. Hata hivyo, Hazem Qassem, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amejibu matamshi hayo ya kijuba ya waziri wa mambo ya nje wa Imarati kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter akisema: Matamshi ya kichochezi ya Abdullah bin Zayed Aal Nahyan dhidi ya HAMAS yanakinza na matukufu na thamani zote za Kiarabu na kitaifa.

Israel inafanya jinai kubwa dhidi ya watu wa kawaida lakini baadhi ya nchi za Kiarabu kama Imarati zinadai kila anayekabiliana na jinai hizi za Wazayuni eti ni gaidi

 

Tukumbuke kuwa, matamshi hayo ya Abdullah bin Zayed Aal Nahyan, waziri wa mambo ya nje wa Imarati ameyatoa kwenye mkutano wa kamati ya Mayahudi wa Marekani uliofanyika kwa njia ya Intaneti. Kwa kweli kujipendekeza kwa Mayahudi ni moja ya malengo makuu ya viongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu. Baada ya kutoa matamshi hayo dhidi ya makundi ya muqawama wa Kiislamu, Imarati imekubaliwa kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa muda wa miaka miwili. Inaonekana wazi kwamba magenge ya Kiyahudi na Kizayuni yana ushawishi mkubwa sana katika siasa na maamuzi ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaani imarati.

Tags