Jun 16, 2021 07:49 UTC
  • Hamas: Mashambulizi dhidi ya Ghaza ni jaribio lililofeli la kuzuia muqawama wa wakazi wa Quds

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Ghaza lilikuwa jaribio lililofeli kwa lengo la kuzuia mapambano ya wananchi wa Palestina katika mji wa Quds.

Msemaji wa Hamas Hazim Qassim ametamka hayo akizungumzia mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ghaza. Ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, hatua ya Wazayuni ya kuushambulia Ukanda wa Ghaza lilikuwa jaribio lililoshindwa la kutaka kuzuia mshikamano na mapambano ya wananchi wa Palestina katika mji wa Quds.  

Qassim amesisitiza kuwa, mashambulizi hayo yalifanywa kwa lengo la kuficha hali mbaya inayoukabili utawala wa Kizayuni katika kuratibu kile kinachotajwa kuwa ni "Maandamano ya Bendera." 

Msemaji wa Hamas ameongeza kuwa, wananchi wa Palestina na wanapambano shujaa wataendelea kuyalinda na kuyatetea matukufu yao hadi pale watakapowafukuza maghasibu katika ardhi yao.  Walowezi wa Kizayuni Jumanne hii walifanya maandamano ya kichochezi kwa jina la Maandamano ya Bendera huko Quds inayokaliwa kwa mabavu. 

Mkabala na hatua hiyo ya walowezi wa Kizayuni, Wapalestina huko Quds, katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza pia wameandamana dhidi ya kitendo hicho cha Wazayuni na kulaani hujuma za utawala huo huko Quds. 

Maandamano katika mji wa Quds 

 

Tags