Jun 17, 2021 02:25 UTC
  • Amnesty yataka uchunguzi wa kifo cha mfungwa wa kisiasa Bahrain

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa mwito wa kufanyika uchunguzi huru wa kifo tatanishi cha mfungwa wa kisiasa huko nchini Bahrain.

Lynn Maalouf, Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesisitiza kuwa, "utawala wa Bahrain unapaswa kuanzisha mara moja uchunguzi huru, usioegemea upande mmoja na athirifu wa mazingira ya kufariki dunia mwanaharakati Hussein Barakat.

Hussein Barakat, ambaye alikuwa mfungwa wa kisiasa alipoteza maisha baada ya kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19 akiwa katika gereza la kuogofya la utawala wa kiimla wa Aal Khalifa.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Amnesty International ameashiria hatua ya utawala wa Manama ya kuendelea kuwanyima wafungwa barakoa na vitakasa mikoni vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona na kueleza bayana kuwa, uchunguzi huru wa kifo cha Barakat unapaswa kubainisha iwapo mwanaharakati huyo alipewa matibabu kwa wakati faafu au la.

Maandamano ya kulaani wa ukatili wa Aal-Khalifa

Barakat alikuwa mwanaharakati wa Kiislamu ambaye alikuwa anashikiliwa katika gereza la kuogofya la Jau kusini mwa Manama ambapo wakuu wa gereza hilo walikataa kumpa matibabu.

Wiki iliyopita katika siku za Jumatano na Alkhamisi, Wabahraini walijitokeza kuandamana katika mji mkuu Manama, kulaani kile walichokitaja kuwa kitendo cha utawala wa Aal Khalifa cha kumuua shahidi mfungwa huyo wa kisiasa ambaye alikuwa Muislamu wa madhehebu ya Shia.

Tangu Februari mwaka 2011, wakati ulipoanza mwamko wa Kiislamu Asia Magharibi, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Tags