Jun 17, 2021 07:21 UTC
  • Uungaji mkono wa Wapalestina kwa Hamas umeongezeka baada ya 'Upanga wa Quds'

Utafiti mpya wa maoni unaonesha kuwa, uungaji mkono wa Wapalestina kwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) umeongezeka zaidi baada ya kujiri vita vya Saif al Quds (Upanga wa Quds).

Utafiti huo uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Sera na Mafunzo ya Kistratajia cha Palestina (Masarat) umeonesha kuwa, asilimi 70 ya watu waliohojiwa wanaitakidi kuwa Hamas iliibuka mshindi katika vita hivyo.

Utafiti huo uliowashirikisha Wapalestina 1,200 wanaoishi katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umebainisha kuwa, asilimia 53 ya waliohojiwa wanaamini kuwa Hamas ina haki ya kuwaongoza na kuwawakilisha wananchi wa Palestina.

Wanamuqawama wa Hamas

Kadhalika utafiti huo umesema kuwa, asilimia 65 ya walioshiriki wanaamini kuwa, kwa kuvurumisha maroketi, Hamas iliulazimisha utawala wa Kizayuni kusitisha harakati zake za kuwafurusha wakazi wa Sheikh Jarrah, mashariki mwa Quds Tukufu.

Vita vya Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ghaza vilianza tarehe 10 Mei mwaka huu na kumalizika tarehe 21 mwezi huo huo baada ya serikali ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuomba kusitisha mapigano na wanamapambano wa Palestina. 

Tags