Jun 18, 2021 06:51 UTC
  • Watetezi wa haki za binadamu Uingereza wamlaumu Johnson kwa kukutana na madikteta wa Bahrain

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Uingereza wamemkosoa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Boris Johnson kwa kukutana kimyakimya na mrithi wa utawala wa kidikteta wa Bahrain.

Msemaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la CAAT, Andrew Smith amesema utawala wa kizazi cha Aal Khalifa nchini Bahrain una historia ndefu na ya kuaibisha ya kufanya ukandamizaji na ukatili na kwamba kitendo cha Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson cha kumkaribisha mrithi wa utawala huo, Salman bin Hamad Aal Khalifa mjini London kinatia kinyaa na ni kielelezo cha kuwaunga mkono madikteta na kudunisha kazi za watetezi wa haki za binadamu. 

Mbunge wa chama cha Liberal Democratic katika Bunge la Uingereza Paul Scriven pia amepinga hatua hiyo ya Boris Johnson na kusema: Inasikitisha kuona kuwa hata taarifa rasmi iliyotolewa na Waziri Mkuu huyo wa Uingereza haikuashiria ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika nchini Bahrain.

Kinyume chake serikali ya London imetoa taarifa ikisema pande hizo mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kiusalama na kidiplomasia. 

Tangu Februari mwaka 2011, wakati ulipoanza mwamko wa Kiislamu Asia Magharibi, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Wabahrain wanataka kuwepo uhuru, uadilifu, kukomeshwa ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.

Tags