Jun 18, 2021 12:31 UTC
  • Hamas: Israel imeshambulia tena Ghaza ili kunyanyua mori wa wanajeshi wake

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema kuwa, shambulio la jana la ndege za utawala wa Kizayuni dhidi ya kambi za muqawama katika Ukanda wa Ghaza ni chokochoko mpya za Israel zilizolenga kunyanyua mori wa wanajeshi wake waliopata kipigo katika mapigano ya hivi karibuni ya siku 12 ya Ukanda wa Ghaza maarufu kwa jina la vita vya "Upanga wa Quds."

Msemaji wa HAMAS, Fauzi Barhoum, amesema hayo leo Ijumaa na kuongeza kuwa, hata adui akifanya upuuzi wowote anaoweza, lakini hawezi kufuta fedheha ya kipigo alichopata katika vita vya siku 12 vya Ghaza kutoka kwa wanamuqawama wa Palestina wakiongozwa na brigedi za Izzuddin Qassam.

Amesisitiza kuwa, kulinda matukufu ya Palestina na ya Kiislamu ni jukumu la kitaifa, kidini na kimaadili na kwamba wanamuqawama wako imara katika azma yao wa kukomboa haki zote za Paletina kwa njia yoyote ile.

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS vile vile amesema, njia za kupambana na adui Mzayuni zinaainishwa na wanamuqawama. Si muda mrefu umepita tangu kumalizika vita vya "Upanga wa Quds" vya siku 12 kwenye Ukanda wa Ghaza ambapo katika vita hivyo, wanamapambano wa Palestina waliweza kumlazimisha adui aombe kusimamishwa vita na kukubali masharti yote ya Wapalestina.

Israel inaingia kiwewe kila inapofikiria makombora ya Wapalestina

 

Wazayuni walilazimika kuomba kusimamishwa vita baada ya kushindwa kuhimili vipigo vikali walivyokuwa wakipokea kutoka katika mashambulizi ya makombora na maroketi ya wanamuqawama wa Palestina.

Jana usiku ndege za utawala wa Kizayuni zilishambulia kwa mara nyingine maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Ghaza ikiwa ni uvunjaji wa wazi wa makubaliano ya kusimamisha vita.

Kuanzia tarehe 10 Mei 2021, utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanya mashambulizi makubwa ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Ghaza huko Palestina kwa muda wa siku 12 na kufanya uharibifu mkubwa sambamba na kuua na kujeruhi idadi kubwa ya Wapalestina wasio na hatia lakini ulichezea kipigo kikali cha makombora na maroketi ya wanamuqawama wa Kiislamu. 

Tags