Jun 20, 2021 08:15 UTC
  • Makundi ya muqawama ya Palestina yautahadharisha utawala wa Kizayuni

Makundi ya muqawama ya Palestina yametangaza kuwa hayautauruhusu utawala ghasibu wa Kizayuni uutwishe muqawama masharti yake au kuufanya Ukanda wa Ghaza uwe katika hali ya kutengwa.

Khodr Habeeb mmoja wa viongozi wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesisitiza kuwa, chumba cha oparesheni za pamoja za makundi ya muqawama kimetangaza msimamo wake wa mwisho kuhusu kukaririwa hatua za Israel katika siku za usoni. Amesema wanamapambano wa Palestina hawatasita kukabiliana na mashambulizi ya utawala huo. 

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Jihad Islami amebainisha kuwa, kuendelea chokochoko na mashambulizi ya Israel kutapelekea kuanza tena makabiliano ya kijeshi katika maeneo ya mipakani na kwamba mashinikizo makubwa ya baadhi ya pande kwa muqawama hayatakuwa maana iwapo mashambulizi yatakaririwa. 

Khodr Habeeb amesema kuwa, kuendelea chokochoko na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kutasambaratisha juhudi za kimataifa zinazoongozwa na Misri kwa ajili ya kudumisha amani na utulivu. Amesema, kitendo cha kutumwa baluni za moto upande wa maeneo ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kinahusiana na kuendelea kuzingirwa eneo la Ukanda wa Ghaza na kufungwa vivuko mbalimbali vya eneo hilo kwa muda wa mwezi mmoja na nusu.  

Amesema wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wanaishambulia Ghaza ikiwa ni hatua ya kimaonyesho kwa shabaha ya kurejesha na hamasa baina ya wanajeshi wa utawala huo waliopoteza matumaini baada ya kipigo cha Ghaza. 

Ndege za kivita na droni za utawala wa Kizayuni Alhamisi iliyopita kwa mara nyingine tena zililishambulia eneo la Ghaza. 

Mashambulizi ya droni na ndege za kivita za Israel Ukanda wa Ghaza 

 

Tags