Jun 20, 2021 12:10 UTC
  • Ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya ScanEagle kama ile iliyotunguliwa na Jeshi la Yemen
    Ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya ScanEagle kama ile iliyotunguliwa na Jeshi la Yemen

Jeshi la Yemen limetangaza kuwa limefanikiwa kutungua ndege ya kijasusi ya Jeshi la Marekani katika anga ya mkoa wa Ma'rib.

Msemaji wa Jeshi la Yemen Yahya Saree aesema ndege hiyo isiyo na rubani au drone iliyotunguliwa ni aina ya Scan-Eagle na ilitunguliwa wakati ikiwa inapaa katika anga ya eneo la Mashjah mkoani Ma'rib.

Ameongeza kuwa drone hiyo ya kisasa kabisa imetunguliwa na wanajeshi wa Yemen waliokuwa wakitumia kombora la nchi kavu kuelekea angani.

Msemajji huyo wa Jeshi la Yemen amesisitiza kuwa, wanajeshi wa Yemen hawatasita hata kidogo katika kutekeleza majukumu yao ya kuilinda anga ya nchi hiyo ili kuzima hujuma za wavamizi.

Msemaji wa Jeshi la Yemen Yahya Saree

Ndege kadhaa zisizo na rubani za Jeshi la Marekani zimetunguliwa na Jeshi la Yemen linaloshirikiana na kamati za wanachi za kujitolea vitani tangu Saudi Arabia ilipoanzisha uvamizi dhidi ya Yemen mwaka 2015.

Saudi Arabia inaungwa mkono kijeshi na Marekani katika uvamizi wake unaoendelea dhidi ya Yemen na ambao umepelekea makumu ya maelfu ya Wayemen kupoteza maisha wengi wakiwa ni wanawake na watoto wasio na hatia.