Jun 21, 2021 02:54 UTC
  • Hamas: Msikiti wa al-Aqsa utakombolewa karibuni hivi

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema taifa la Palestina karibuni hivi litaukomboa Msikiti mtukufu wa al-Aqsa, huko Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu.

Yahya al-Sinwar alisema hayo jana Jumapili katika kongamano la kuiunga mkono kambi ya muqawama na Qud tukufu na kuongeza kuwa, makundi yote ya Palestina yatapata ushindi na kuikomboa Baitul Muqaddas.

Sinwar amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la Shehab na kueleza bayana kuwa, Wapalestina wote wamekaribia sana kuukomboa Masjidul Aqsa na muda si mrefu wataswali kwenye Msikiti huo.

Kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Hamas amesisitiza kuwa, msimamo wa Wapalestina juu ya kuukomboa Msikiti wa al-Aqsa haujabadilika licha ya baadhi ya tawala za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Shambulio la Wazayuni dhidi ya Masjidul Aqsa

Hii ni katika hali ambayo, walowezi wa Kizayuni jana Jumapili waliuvamia Msikiti huo wa al-Aqsa na kulivunjia heshima eneo hilo takatifu, huku wakipewa himaya ya askari wa utawala haramu wa Israel wakati wakitekeleza jinai hiyo.

Mapema mwezi huu pia, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon alisema hakuna chembe ya shaka kuwa Waislamu wote karibuni hivi wataibuka washindi mkabala wa Wazayuni na waitifaki wao, na hatimaye watatekeleza ibada ya Swala katika Msikiti mtukufu wa al-Aqsa.

Tags