Jun 21, 2021 11:59 UTC
  • Maiti za watoto wa Palestina waliouawa na Israel
    Maiti za watoto wa Palestina waliouawa na Israel

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Palestina imeukosoa Umoja wa Mataifa kwa kutoiweka Israeli kwenye orodha nyeusi ya kila mwaka ya makundi na nchi zinazohusika na ukiukaji mkubwa wa haki za watoto, ikisema kupuuza jinai za utawala huo kunawapa kinga ya kuhukumiwa Wazayuni wanaoua watoto.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema: "Hatua ya Umoja wa Mataifa ya kutouweka utawala wa Kizayuni wa Israel katika orodha nyeusi ya serikali na makundi yanayokiuka haki za watoto katika mizozo ya silaha ni kumpendelea muuaji na kuwaunga mkono wahalifu wa jeshi la Kizayuni na walowezi magaidi, na inawakingia kifua ili wasichukuliwe hatua."

Taarifa hiyo imesema, hatua ya UN inaziweka ripoti zake katika hatari ya " ya kutambuliwa kuwa ni batili" na "zisizokuwa na uaminifu"; na inazusha shaka na maswali mengi kuhusu misingi na kanuni za umoja huo.

Katika ripoti ya hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliitaka Israeli kupunguza mashambulizi ya jeshi dhidi ya watoto wa Palestina na kuhakikisha adhabu inatolewa kwa wanajeshi wake wanaouawa watoto. Hata hivyo Antonio Guterres aliamua kutoliweka jina la Israel katika orodha ya makundi na tawala zinazokiuka haki za watoto licha ya kuua makumi ya watoro wadogo wa Palestina. 

Kinyume chake Umoja wa Mataifa uliiweka Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen katika orodha ya makundi yanayokiuka haki za watoto lakini wakati huo huo haikuziweka Saudi Arabia na utawala haramu wa Isrel zinazoua watoto wa Yemen na Palestina katika orodha hiyo.   

Awali Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ilikuwa imetangaza kuwa, hatua ya Umoja wa Mataifa ya kutoliweka jina la utawala wa Kizayuni wa Israel katika orodha ya wakiukaji wa haki za watoto ni sawa na kubariki jinai zinazofanywa na utawala huo.

Hamas imesema kuwa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel za kuua, kusweka watu jela, kuteka nyara, kutokuwepo uchunguzi wa wazi kuhusu jinai na uhalifu unaofanywa na utawala huo na jinai ya karibuni ya kuua watoto 66 wasio na hatia katika mashambulizi yake dhidi ya Gaza na mauaji ya watoto yanayofanywa na Israel kila uchao katika barabara na mitaa ya Ukingo wa Magharibi vinatosha kuliweka jina la Israel katika orodha ya wakiukaji wa haki za watoto duniani. 

Vilevile harakati ya Ansullah ya Yemen imesema kuwa, Guterres amethibitisha kuwa, Umoja wa Mataifa ni jukwaa lisilo na thamani yoyote ambalo linatumiwa na nchi zenye ushawishi mkubwa duniani kwa ajili ya kupotosha ukweli na kukanyaga haki za mataifa yanayokandamizwa. 

Maelfu ya watoto wa Yemen wameuwa katika mashambulizi ya Saudi Arabia

Taarifa iliyotolewa na Ansarullah imesema kuwa, ilikuwa vyema UN iwe taasisi isiyopendelea upande wowote na isikariri bwabwaja za muungano vamizi huko Yemen. 

Tags