Jun 22, 2021 02:31 UTC
  • Uporaji wa mali ya Syria na Iraq, sababu ya mashinikizo ya wananchi ya kutaka wavamizi wa Kimarekani waondoke

Kuwepo kwa majeshi vamizi ya Marekani katika eneo lolote la Magharibi mwa Asia na hata maeneo mengine ya dunia daima kumekuwa sababu ya ukosefu wa amani na mashaka na machungu kwa wakazi wa maeneo hayo, tofauti kabisa na madai yanayotolewa na serikali ya Washington.

Kwa miaka kadhaa sasa wanajeshi vamizi wa Marekani, mamluki na wanamgambo wa makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na serikali ya Washington na washirika wake wamevamia maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Syria na vilevile kaskazini mwa Iraq, na licha ya wito wa serikali za nchi hizo zinazoitaka Marekani iondoke katika maeneo hayo yanayokaliwa kwa mabavu, lakini wavamizi hao wameendelea kuwepo katika ardhi ya nchi hizo na kupota utajiri na rasilimali zao kama za mafuta, gesi na mazao ya kilimo. Hii ni pamoja na kuwa, wakazi wa maeneo hayo yaliyovamiwa na Marekani na mamulki wake wanaendelea kusumbuliwa na mashinikizo na matatizo mengi ya kiuchumi ya kijamii. 

Katika uwanja huo televisheni ya al Ikhbariyya ya Syria Jumatatu ya jana ilifichua jinsi wanajeshi hao vamizi wa Marekani wanavyoendelea kupora utajiri na rasilimali za nchi hiyo. Ripoti iliyotolewa na televisheni hiyo imesema kuwa: Wanjeshi vamizi wa Marekani wanashirikina na wapiganaji wa kundi la kigaidi la SDF katika kuiba ngano na mafuta ya Syria kwa kadiri kwamba, hivi karibuni tu wanajeshi hao walisafirisha malori 32 yaliyokuwa yamesheheni ngano kutoka maeneo ya kaskazini mwa Syria na kuyapeleka kwenye kambi yao iliyoko kaskazini mwa Iraq. Mwezi uliopita wa Mei pia wanajeshi hao wa Marekani walipora malori 150 yaliyokuwa yamebeba ngano na magari zaidi ya 500 ya kubeba mafuta ya Syria na kuyapelekea kwenye kambi zao. 

Msafara wa wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Syria

Moja kati ya malengo ya hatua hizo za Marekani ni kudhamini mahitaji ya wanajeshi wake huko kaskazini mwa Syria na Iraq na vilevile kukidhi mahitaji ya mamluki na vibaraka wake kama kundi la SDF na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Jabhatu Nusra. Wizi na uporaji huo wa mali na utajiri wa watu wa Syria unaendelea kufanywa na majeshi vamizi ya Marekani huku wakazi wa maeneo hayo hasa eneo la Manbij wakiendelea kuwasilisha mashtaka na malalamiko yao hata kwa Marekani yenyewe juu ya uhalifu mkubwa unaofanywa na makundi hayo ya kigaidi yanayofadhiliwa na serikali ya Washington. Wiki kadhaa zilizopita pia makabila ya Kiarabu ya mkoa wa Aleppo (Halab) yalitangaza kuwa, yako tayari kwenda kuwahami wakazi wa Manbij na kusisitiza udharura wa kuungana makabila yote ya eneo hilo kwa ajili ya kukabiliana na wanamgambo wa kundi la SDF linalosaidiwa na Marekani.

Kwa kuzingatia hayo yote na kutokana na kuchoshwa na uhalifu huo, wakazi wa maeneo ya kaskazini mwa Syria na Iraq wanataka wanajeshi vamizi wa Marekani waondoke katika ardhi za nchi zao, na si ajabu tukashuhudia mashambulizi ya raia hao dhidi ya vituo na kambi za wanajeshi hao huko Syria na Iraq. Raia hao pia wanapinga hatua ya Marekani ya kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wapiganaji wa makundi ya kigaidi kama Daesh ambao wanatumiwa kushambulia vituo na kambi za jeshi la Syria na taasisi za kiraia za nchi hiyo.

Wanajeshi wa kigaidi wa Marekani Iraq

Katika mkondo huo huo duru za kuaminika nchini Iraq zimeripoti kuwa, kambi za wanajeshi wa Marekani za al Al-Shaddadeh na Al-Hasakah huko kaskazini mwa Syria jana Jumatatu zilishambuliwa kwa maroketi.

Ukweli ni kwamba, watu wa Iraq na Syria wanataka kuondoka wanajeshi vamizi wa Marekani katika nchi zao na matakwa hayo halali yanapaswa kupewa mazingatio.   

Tags