Jun 27, 2021 02:37 UTC
  • Palestina yataka kuwekwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Israel

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Palestina imelaani uhalifu unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Palestina na kutoa wito wa kuwekwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala huo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Palestina imetangaza kuwa, utawala vamizi wa Israel unaendelea kupuuza ripoti za mashirika ya kimataifa yanayosisitiza kuwa, Tel Aviv imefanya dhulma na ubaguzi mkubwa zaidi dhidi ya Wapalestina. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, upinzani wa nchi na jumuiya za kimataifa dhidi ya ubaguzi na dhulma kubwa za Israel huko Palestina unapaswa kufuatiwa na vitendo; hivyo taasisi za kimataifa zinalazimika kuwatetea Wapalestina wanaodhulumiwa na kutekeleza maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala hilo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema Marekani na Umoja wa Ulaya zinaupendelea na kuukingia kifua utawala wa Kizayuni wa Israel na hazijachukua hatua yoyote ya kuzuia mauaji, mateso, dhulma na wizi wa ardhi ya Palestina unaofanywa na utawala huo ghasibu. 

Mwishoni mwa mwezi uliopita nchi 63 zililitaka Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lifanye uchunguzi na kushughulikia jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wasio na hatiai wa Palestina.

Wanajeshi wa Israel wakiwanyanyasa Wapalestina

Raia zaidi ya 250 wa Palestina waliuawa katika hujuma na mashambulizi ya pande zote yaliyofanywa na jeshi la Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza mwezi uliopita wa Mei. 

Vilevile shirika la kutetea haki za bindamu la Human Rights Watch ambalo ni taasisi isiyo ya serikali yenye makao yake mjini New York huko Marekani, mwishoni mwa Aprili mwaka huu wa 2021 lilitoa ripoti yenye kurasa 213 ambayo likiitambua Israel kuwa ni utawala wa ubaguzi wa Apartheid na kuitaka Mahakama ya Kimaaifa ya Jinai (ICC) kuufikisha mahakamani utawala huo ghasibu.   

Tags