Jul 07, 2021 11:10 UTC
  • Mtazamo wa Sayyid Hassan Nasrallah kuhusu duru mpya ya vita vya Marekani dhidi ya muqawama kupitia vyombo vya habari

Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Jumatatu alitoa hotuba akiashiria hatua ya Marekani kuteka na kufunga tovuti za habari zinazofungamana na harakati za muqawama au mapamabano ya Kiislamu ambapo ametoa sababu kadha za uhasama huo wa Marekani.

Ikumbukwe kuwa tarehe 22 Juni, Wizara ya Sheria ya Marekani iliendeleza sera za kiijuba na kibeberu za nchi hiyo kwa kuzifunga tovuti za televisheni za kimataifa za Iran na vyombo vya habari vya mrengo wa mapambano ya Kiislamu vya Yemen, Palestina, Iraq na Bahrain. Televisheni ya Kiingereza ya Iran ya Press TV na zile za Kiarabu za Al Alam na Al Khauthar ni kati ya vyombo vya habari ambavyo vimefungiwa tovuti zao na Marekani kwani zilikuwa zinaishia na kikoa cha .com ambacho humilikiwa na shirika moja la Kimarekani. Kitendo hicho kimelaaniwa kote duniani na kutajwa kuwa ukiukaji wa wazi wa uhuru wa maoni.

Sayyid Hassan Nasrullah ambaye alikuwa akizungumza Juni 5 mjini Beirut kwa njia ya televisheni katika ufunguzi wa mkutano wa "Palestina Itashinda" aliashiria hatua hiyo ya Marekani na kutaja sababu tatu ambazo zimepelekea Marekani iteke tovuti za vyombo hivyo vya habari. Sababu hizo ni pamoja na kuwa vyombo hivyo vya habari vinafichua ukweli, vinaaminika na vina athari kubwa na hivyo vimekabaliwa na duru mpya ya vita vya Marekani dhidi ya vyombo huru vya habari.

Sayyid Hassan Nasrallah amesema vyombo hivyo vya habari vya mrengo wa muqawama vimekuwa vikifichua utambulisho wa sera za Marekani katika eneo la Asia Magharibi. Kuhusu nukta hii ameashiria nukta mbili za kadhia ya fitina ya ISIS au Daesh na nafasi ya Marekani katika sera za utawala wa Kizayuni wa Israel. Katibu Mkuu wa Hizbullah anaamini kuwa, "Fitina ya Daesh ilikuwa na lengo la kupelekea kadhia ya Palestina isahaulike." Vyombo vya habari vya mrengo wa muqawama au mapambano ya Kiislamu viliweza kudiriki njama hiyo na hivyo vikaweza kuifichua na hatimaye kuisamabaratisha.

Katibu Mkuu wa Hizbullah aidha amesema hujuma ambazo zinatekelezwa na Israel dhidi ya Palestina na nchi zingine zinatekelezwa kwa uungaji mkono kamili wa Marekani ambapo katika kadhia hii vyombo vya habari vya muqawama vimweza kufichua ukweli wa namna Marekani ilivyo mshirika katika jinai za Israel. Sayyid Nasrallah amasema: "Sera za mrengo wa muqawama zimejengeka katika misingi ya kubainisha ukweli na uhalisia wa mambo katika medani, hisiasa za mataifa na utambulisho wa adui. Sisi tunafahamu nukta dhaifu za adui na tunaachukua hatua za kukabiliana naye na kumdhoofisha.".

Kwa mtazamo wa Sayyid Nasrallah, sababu nyingine ya hatua za Marekani dhidi ya tovuti za habari za mrengo wa muqawama ni kuwa  vyombo vya habari vya muqawama vinatangaza habari zinazoaminika na wengi.  Kwa maneneo mengine ni kuwa vyombo vya habari vya mrengo wa harakati za Kiislamu hutangaza habari na taarifa zinazofichua sura halisi ya Marekani na habari hizo huaminika na hivyo kupelekea ushawishi wa Marekani kupungua sana katika mataifa ya eneo. Aidha kuaminika vyombo vya habari vya muqawama kumepelekea Marekani ifeli katika vita vyake  vya kisaikolojia dhidi ya mrengo wa muqawama. Katibu Mkuu wa Hizbullah ameashiria kufeli adui katika vita vya kisaikolojia na kusema: "Sisi katika vita vyetu vya kisaikolojia hatudanganyi wala kuhadaa kwani moja ya nukta zenye nguvu katika vyombo vya habari vya muqawama ni kuwa vinasema ukweli wa mambo."

Mtandao wa Kimarekani wa  YouTube pia umezuia Press TV kuweka video zake katika jukwaa hilo

Nukta ya tatu ambayo Sayyid Hassan Nasrallah ameashiria kuhusu kitendo cha Marekani kufunga tovuti za vyombo vya habari vinavyofungamana na mrengo wa muqawama au mapambano ya Kiislamu ni kuwa, vyombo hivi vya habari vimekuwa na taathria kubwa. Ni wazi kuwa, adui daima anajaribu kuharibu taswira ya mrengo wa muqawama. Kwa mfano adui daima huiarifisha harakati ya Hizbullah kama chanzo cha matatizo. Nchini Iraq Harakati ya Hashd al Shaabi nayo pia inahujumiwa kama amavyo pia nchini Yemen Harakati ya Ansarullah inalaumiwa kuwa eti ni chanzo cha kuendelea vita nchini humo. Propaganda hizo zimekuwa zikienezwa katika vyombo vya habari vya adui. Lakini si tu kuwa vyombo vya habari vya mrengo wa muqawama vimeweza kufanikiwa katika kukabiliana na propaganda hizo chafu bali pia vimekuwa na nafasi muhimu katika ushindi wa harakati za muqawama. Kuhusiana na nukta hii, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: 'Adui ameamua kufunga televisheni za satalaiti na tovuti za intaneti za mashirika ya habari ya muqawama kutokana na athari kubwa ya vyombo hivyo vya habari."

Tags