Jul 09, 2021 12:38 UTC
  • Mfalme wa Jordan aonana na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimetangaza kuwa, mfalme wa Jordan ameonana na waziri mkuu wa Israel katika mji mkuu Amman.

Mtandao wa habari wa Kizayuni unaojulikana kwa jina la Walla umeripoti habari hiyo leo Ijumaa na kumnukuu afisa mmoja wa zamani wa serikali ya Israel akisema kuwa, mfalme wa Jordan, Abdullah wa Pili, alionana na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Naftali Bennet mjini Amman wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa tovuti hiyo ya Kizayuni, katika mazungumzo yao hayo, pande mbili zimekubaliana kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa Amman na utawala wa Kizayuni.

Naftali Bennet, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni

 

Katika mazungumzo hayo, Bennet alimwambia Abdullah wa Pili kwamba utawala wa Kizayuni umekubaliana na mpango kuiuzia Jordan kiwango kikubwa zaidi cha maji.

Kabla ya hapo pia, ofisi ya mfalme wa Jordan ilikuwa imetangaza kuwa, waziri wa mambo ya nje wa Jordan, Ayman Safadi alikuwa ameonana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Israel, Yair Lapid na pande mbili zikakubaliana kwamba utawala wa Kizayuni uiuzie Jordan mita mraba milioni 50 za ziada za maji ambayo tayari yameshalipiwa tangu zamani. 

Utawala wa Kizayuni unatumia vyanzo vya maji unavyovikalia kwa mabavu kuzishinikiza nchi za eneo hili, wala dunia haisemi kitu. Lakini inapotokezea nchi fulani ya Kiislamu na Kiarabu kutangaza kutumia nishati ya mafuta kushinikiza matakwa yake, dunia nzima inapiga makelele na kudai kuwa si ubinadamu kutumia maliasili kama wenzo wa mashinikizo.

Tags