Jul 10, 2021 12:18 UTC
  • Askari wa Kizayuni wawafyatulia risasi na kuwajeruhi mamia ya Wapalestina

Askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wamewafyatulia risasi na kuwajeruhi mamia ya Wapalestina waliokuwa wakiandamana kulalamikia ujenzi haramu wa kituo cha jeshi hilo ghasibu katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu.

Wapalestina zaidi ya 370 wamejeruhiwa katika makabiliano hayo, wakiwemo 31 waliojeruhiwa kwa risasi za moto.

Jeshi la utawala haramu wa Kizayuni limetumia pia droni kunyunyiza gesi ya kutoa machozi na moshi katika mji wa Beita ulioko karibu na Nablus, ambako mamia ya Wapalestina waliandamana jana kulalamikia unyakuzi haramu wa ardhi yao.

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limethibitisha kuwa Wapalestina 371 wamejeruhiwa, 31 miongoni mwao kwa risasi za moto, katika maandamano hayo yaliyofanyika katika mji wa Beita baada ya Sala ya Ijumaa.

Makabiliano mengine kati ya askari wa jeshi la utawala haramu wa Kizayuni na Wapalestina yalitokea pia katika mji wa Kafr Qaddum na Beit Dajan ambapo makumi ya waandamanaji walishambuliwa kwa mabomu ya kutoa machozi.

Askari wa Kizayuni wakiwafyatulia mabomu ya kutoa machozi Wapalestina

Jeshi la utawala wa Kizayuni liliwakandamiza pia waandamanaji waliokuwa wakipinga na kulalamikia ujenzi haramu wa vitongoji katika eneo la Masafer Yatta karibu na Hebron.

Kuna walowezi wa Kizayuni wapatao 650,000 wanaoishi kwenye vitongoji 164 na vituo vya kijeshi 116 katika eneo la Ufukwe wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Baitul Muqaddas Mashariki.

Ujenzi wa vitongoji vyote hivyo unaofanywa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel unatambuliwa kuwa ni haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.../

 

Tags