Jul 11, 2021 13:24 UTC
  • Al Qaeda yaungama hadharani kuwa inapigana bega kwa bega na Muungano wa Saudia Yemen

Mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda umetoa taarifa ukikiri kwamba, katika vita vinavyoendelea katikati ya Yemen unapigana bega kwa bega na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya vikosi vya jeshi la Yemen na vile vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo.

Baada ya kutolewa ripoti nyingi zilizoonyesha kuwa muungano wa kijeshi wa Saudia unasaidiwa kijeshi na wanamgambo wa genge la kigaidi la Al Qaeda katika vita vya Yemen, hatimaye genge hilo limetoa taarifa kuthibitisha ukweli wa ripoti hizo.

Katika taarifa yake hiyo, Al Qaeda imetangaza kuwa, imekuwa ikipigana bega kwa bega na vikosi vya muungano wa kijeshi wa Saudia katika vita vya maeneo ya As-Sum'a na Az-Zaahir mkoani Al Baydhaa katikati mwa Yemen.

Hivi karibuni, jeshi la Yemen lilifanikiwa kuyakomboa maeneo muhimu katika medani za mapigano kwenye mkoa wa Al Baydhaa kupitia shambulio la kushtukiza dhidi ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia.

Abdulmalik al Ajri, mjumbe wa timu ya mazungumzo ya serikali ya uwokovu wa kitaifa ya Yemen, naye pia ametangaza kuwa, Marekani inapigana bega kwa bega na makundi ya kigaidi ya DAESH (ISIS) na Al Qaeda, lakini hakuna mtu yeyote anayezungumzia hilo; kama ambavyo Al Qaeda imepigana bega kwa bega na muungano vamizi wa Saudia katika maeneo ya Al Baydhaa, Tai'z na mengine kadhaa, lakini Marekani inalifumbia macho suala hilo.../

 

Tags