Jul 12, 2021 03:40 UTC
  • Sultan Haitham awasili Saudia katika safari ya kwanza ya kiongozi wa Oman baada ya kupita zaidi ya miaka 10

Sultan Haitham bin Tarik wa Oman amefanya safari ya kwanza nje ya nchi kwa kuitembelea Saudi Arabia, ikiwa pia ni mara ya kwanza kufanywa na kiongozi mkuu wa Oman huko Riyadh baada ya kupita zaidi ya muongo mmoja.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, Sultan Haitham bin Tarik aliwasili nchini Saudia jana Jumapili kwa ziara ya siku mbili kuitikia mwaliko rasmi aliopewa na Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Saudi Arabia SPA, katika uwanja wa ndege, Sultan wa Oman alilakiwa na mrithi wa ufalme wa Saudia Mohammad bin Salman pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo akiwemo waziri wa mambo ya ndani na balozi wa Saudia nchini Oman.

Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia (mwenye fimbo) akimkaribisha Sultan Haitham bin Tarik wa Oman

Imeelezwa kuwa, ziara hiyo rasmi ya Sultan Haitham bin Tarik nchini Saudi Arabia inalenga kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na kupanua wigo wa ushirikiano na njia za kuustawisha katika nyanja mbalimbali kwa ajili ya hali bora ya maisha na ustawi wa wananchi wa nchi hizo mbili.

Kadhalika, mazungumzo ya viongozi wa nchi hizo mbili yameelezwa kuwa ni mwendelezo wa harakati za kidiplomasia zinazofanywa na Sultan wa Oman kwa madhumuni ya kuyapa msukumo mazungumzo ya amani ya Yemen kulingana na mapatano yaliyofikiwa kikanda na kimataifa kwa lengo la kuhitimisha vita vya miaka saba na kuzikutanisha katika mazungumzo ya ana kwa ana pande husika katika vita hivyo.../

Tags