Jul 12, 2021 04:10 UTC
  • Umuhimu wa ushindi wa jeshi la Yemen katika mapambano ya mkoa wa al Bayda'

Jeshi la Yemen kwa kushirikiana na kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiyo maarufu kuwa jina la Ansarullah limepata ushindi mkubwa na muhimu dhidi ya magaidi wa al Qaida na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia kwenye mkoa wa al Bayda'.

Katika kipindi cha siku za hivi karibuni, mkoa wa al Bayda' umekuwa medani kubwa ya mapambano. Magaidi wa al Qaida walikuwa wamejiimarisha vizuri katika mkoa huo. Ndio maana jeshi la Yemen kwa kushirikiana na kamati za kujitolea za wananchi limeamua kuusafisha mkoa huo na uwepo wa magaidi hao. Vita vikali vimetokea na hadi hivi sasa jeshi la Yemen kwa kushirikiana na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen limepata ushindi mkubwa na limewalazimisha magaidi wa al Qaida kukimbia.

Abdul Wahhab al Hamiqani, mmoja wa viongozi wa genge la al Qaida ametumia mtandao wa kijamii wa Twitter kukiri kushindwa magaidi hao mbele ya wanajeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen na kuandika: Askari wa San'a wamefanikiwa kudhibiti kikamilifu medani ya al Zahra. Wapiganaji wetu wamelazimika kurudi nyuma na kurejea sehemu walikokuwa kabla.

Wavamizi wa Yemen hawajapata chochote zaidi ya vipigo vya mtawalia. Picha ya mamluki wa Saudia waliouawa nchini Yemen

 

Mapigano ya mkoa wa al Bayda' yamedhihirisha wazi uhusiano mkubwa na wa karibu uliopo baina ya magenge ya kigaidi kama al Qaida na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia. Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel nao umeshiriki kikamilifu kuwasaidia magaidi wa al Qaida na wavamizi wa Yemen katika vita vya mkoa wa al Bayda' lakini pamoja na hayo vikosi vya San'a vimetoa pigo kubwa kwa wavamizi wote hao wa Yemen.

Hivi karibuni, Kaimu Mkuu wa Majeshi ya Yemen alisema kuwa, wanajeshi wa Marekani ndio wanaoongoza vita katika mkoa wa al Bayda' wakishirikiana na magaidi wa al Qaida, Daesh (ISIS) na Jabhat al Nusra.

Shirika la habari la SABA la Yemen lilitangaza habari hiyo na kumnukuu Meja Jenerali Ali Hamud al Mushki, akifichua uhakika huo na kuongeza kuwa, wakati wanajeshi wa Marekani walipochukua jukumu la kuongoza vita dhidi ya wanajeshi wa Yemen katika mkoa wa al Bayda', wananchi na jeshi la Yemen limevunja jeuri na majigambo ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wanaoongoza vibaraka na mamluki wao kufanya jinai dhidi ya wananchi wa Yemen.

Baada ya hapo pia, yaani siku ya Ijumaa, Msemaji wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Yemen maarufu kwa jina la Ansarullah alisema kuwa, askari wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia wamepata kipigo kikali katika mkoa wa al Bayda' kutoka kwa jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo. Shirika la habari la ISNA lilimnukuu Mohammad Abdul Salaam akisema kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, muungano vamizi unaoongozwa na Saudia haujapata chochote ghairi ya kipigo katika medani zote na kwenye viwango vyote.

Wavamizi wa Yemen wanaposhindwa kwenye medani za mapambano, humalizia hamaki zao kwa wananchi wa kawaida hasa watoto wadogo

 

Ukweli ni kuwa, lengo hasa la wanamapambano wa Yemen wanaopigania ukombozi wa ardhi zote za nchi hiyo, ni kuukomboa kikamilifu mkoa wa Ma'rib. Wavamizi wa Yemen walikuwa wakipata nguvu kupitia mkoa wa al Bayda', sasa; kusafishwa magaidi makatili katika mkoa huo, kumelifungulia njia jeshi la Yemen na Ansarullah kuukomboa kwa urahisi zaidi mkoa wa Ma'rib. 

Suala jingine ni umuhimu wa kiistratijia wa mkoa wa al Bayda' ambao umezungukwa na mikoa minane mikubwa ya Yemen ambayo ni San'a, Dhamar, Ma'rib, Ibb Kaskazini, Lahij, Abyan, Shabwah na Dhale Kusini. Magaidi wa al Qaida walikuwa wakiutumia mkoa wa al Bayda' kuishinikiza mikoa yote hiyo. 

Jengine ni kwamba ushindi wa Jeshi la Yemen na Ansarullah huko al Bayda'  una taathira kubwa za moja kwa moja za kiroho na kisaikolojia kwa jeshi na wanamapambano wa Ansarullah kama ambavyo umezidi kuwavunja moyo magaidi wa al Qaida na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia, Marekani, na utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Tags