Jul 13, 2021 02:36 UTC
  • Jihad al Islami: Muqawama ndiyo njia pekee ya kupambana na Israel

Msemaji wa Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina amewapongeza wanamapambano wa Palestina wanaojihami kwa silaha mbele ya jinai za Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusema kuwa, hiyo ndiyo njia pekee ya kupambana na Israel.

Kwa mujibu wa Falastin al Yaum, Tariq Salami amesema hayo akisisitiza kuwa, jukumu la wanamapambano wa Palestina ni kubeba silaha na kupambana kishujaa na adui Mzayuni.

Ameongeza kuwa, Wazayuni hawatosita kushambulia vitongoji, vijiji na kambi za wakimbizi wa Kipalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hivyo cha kufanya si kuwaomba wasimamishe, bali ni kuwalazimisha Wazayuni wakomeshe jinai zao na hilo haliwezekani ila kwa kutumia mtutu wa bunduki. Amesema, hivi sasa fikra ya kupambana na Israel kwa kutumia silaha imepata nguvu sana Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na hilo ni jambo la kupongezwa kwani litawafanya Wazayuni wafikirie mara mbilimbili kabla ya kufanya jinai yao dhidi ya Wapalestina.

Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan

 

Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni na kutokana na Wazayuni maghasibu kuzidisha jinai zao dhidi ya Wapalestina wasio na hatia kwa kutumia wanajeshi makatili wa Israel, wanamapambano wa Palestina sasa nao wameamua kutumia silaha huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds, ili kujihami mbele ya jinai za Wazayuni.

Kabla ya hapo baadhi ya makundi ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yalikuwa yanapinga matumizi ya silaha na yaliingia tamaa ya kufanikiwa mazungumzo ya mapatano baina yao na utawala wa Kizayuni. Hivi sasa makundi hayo yanakiri kuwa yamefanya kosa kubwa, kwani Israel haina mwamana hata kidogo. 

Tags