Jul 14, 2021 04:07 UTC
  • Duru za kuaminika: Muhammad bin Nayef mahututi, anaweza kufa wakati wowote

Mrithi wa zamani wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Nayef anayeshikiliwa mahabusu ameripotiwa kuwa katika hali mbaya na mahututi na kwamba anaweza kufariki dunia wakati wowote,

Muhammad bin Nayef alikuwa mrithi wa ufalme wa Saudia tangu Januari mwaka 2015 hadi Januari 2017 wakati alipouzuliwa na Mfalme Salman bin Abdulaziz katika kile kilichotambuliwa na wengi kuwa ni mapinduzi baridi, na kumsimika mwanaye, Muhammad bin Salman. 

Mwezi Machi mwaka jana utawala wa Saudi Arabia ulimtia nguvuni Muhammad bin Nayef na ami yake, Ahmad bin Abdulaziz kwa tuhuma za kufanya uhaini na kuwekwa mahabusu. 

Televisheni ya Marekani ya NBC imeripoti kuwa, Bin Nayef ameteswa sana kwa kadiri kwamba, hawezi kutembea bila ya msaada wa watu wengine. 

Mtandao unaofichua habari za ndani ya utawala wa kifalme wa Saudia wa al A'hdul Jadid umeripoti kuwa, mrithi huyo wa zamani wa kiti cha ufalme wa Saudia anasumbuliwa sana na maradhi ya kisukari na amenyimwa huduma za matibabu; suala ambalo limemfanya apoteze kilo 22. Vilevile anasumbuliwa na unyogovu mkali na matatizo ya kinafsi. Mtandao huo umesema hali ya Bin Nayef ni mbaya sana na yumkini akafariki dunia wakati wowote.

Bin Nayef

Mtandao wa A'hdul Jadid umeongeza kuwa: "Kinachoendelea kuhusiana na Muhammad bin Nayef ni 'operesheni ya mauaji ya taratibu', lengo likiwa ni kuonyesha kwamba, kifo chake kilikuwa cha kawaida, na kwamba hakukuwa na agizo la moja kwa moja la kumuua.

Tangu alipoteuliwa kuwa mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman alianzisha operesheni kubwa ya kuwamaliza kabisa wapinzani na wakosoaji wa utawala huo wa kifalme ikiwa ni pamoja na kuwanyonga wapinzani wa ndani, kuwasweka jela, mateso na hata kutuma timu za mauaji katika nchi za nje kwa ajili ya kuwamaliza na kuwaua wapinzani.   

Tags