Jul 15, 2021 08:12 UTC
  • Licha ya kauli kali zitolewazo dhidi ya Wazayuni, marais wa Uturuki na Israel wataka kustawishwa uhusiano

Chama tawala nchini Uturuki cha Uadilifu na Maendeleo AKP kimesema, Uturuki na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel zimekubaliana kuchukua hatua ili kustawisha uhusiano wao wenye mivutano kufuatia mazungumzo yaliyofanywa kwa njia ya simu kati ya marais wa pande hizo mbili.

Siku ya Jumatatu Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais mpya wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Isaac Herzog ili kumpongeza kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Msemaji wa chama cha AKP Omer Celik ameeleza katika taarifa aliyotoa baada ya mkutano wa chama hicho kwamba umeandaliwa utaratibu kufuatia mazungumzo hayo ya simu wa kuhakikisha hatua zinapigwa katika masuala kadhaa kwa lengo la kutatua kadhia zenye matatizo.

Celik amesema, Palestina ni moja ya kadhia ambazo Uturuki inataka kuijadili na Israel.

Erdogan

Licha ya malumbano ya maneno ambayo yamekuwa yakishuhudiwa baina ya Rais Erdogan wa Uturuki na viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel hususan aliyekuwa waziri mkuu wa muda mrefu wa utawala huo Benjamin Netanyahu, Ankara na Tel Aviv zina uhusiano mkubwa wa kibiashara kati yao.

Katika mazungumzo hayo ya simu kati ya marais wa Uturuki na Israel ambayo yamefanyika baada ya Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuitembelea Uturuki, Erdogan amemueleza Herzog kwamba anathamini kuendelezwa mazungumzo na kuongeza kuwa uhusiano wa Uturuki na Israel ni muhimu kwa uthabiti wa eneo.

Rais wa Uturuki anaunga mkono suluhisho la mgogoro kati ya Israel na Wapalestina kupitia uundaji wa mataifa mawili.../ 

Tags