Jul 15, 2021 10:53 UTC
  • Bin Salman atekeleza njama ya kumuangamiza mrithi wa zamani wa kiti cha ufalme huku dunia ikiwa imekaa kimya

Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na habari za kuzorota hali ya haki za binadamu na kuongezeka mateso katika jela za kuogofya za utawala wa Saudi Arabia, moja ikiwa inahusiana na mateso makali dhidi ya Mohammad Bin Nayef, mrithi wa zamani wa ufame wa Saudia.

Pamoja na kuwepo taarifa hizo, kunashuhudiwa kimya cha jamii ya kimataifa hasa taasisi za haki za binadamu zinazofungamana na Umoja wa Mataifa na nukta hiyo inaashiria uwezekano wa kuwepo ushirikiano baina ya taasisi hizo za kimataifa na utawala dhalimu wa Saudia.

Siku ya Jumanne, baadhi ya duru za habari zilidokeza kuwa, mrithi wa zamani wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Nayef aliyeuzuliwa nafasi hiyo na ambaye sasa anashikiliwa mahabusu yuko katika hali mbaya na mahututi na kwamba anaweza kufariki dunia wakati wowote.

Bin Nayef anaripotiwa kuugua ugonjwa wa kisukari shadidi na wala hapokei dawa na jambo hilo limepelekea apungue uzito kwa kiasi kikubwa na pia amekumbwa na matatizo ya kiakili kutokana na mateso makubwa anayoyapata.

Mfalme wa Saudia Mfalme Salman bin Abdulaziz (kushoto) na mwanae, Mohammad bin Salman

Mrithi huyo wa zamani wa ufalme wa Saudia, ambaye kisheria ndiye anayepaswa kuendelea kushikilia wadhifa huo, aliuzuliwa Januari 2017 kufuatia amri ya Mfalme Salman bin Abdulaziz na sahemu yake kuchukuliwa na mwanae Salman, Mohammad bin Salman ambaye ni kijana mwanagenzi asiye na busara. 

Mwaka 2020, Bin Nayef na mjomba wake, Ahmad bin Abdulaziz walikamatwa na kuswekwa gerezani kwa tuhuma za kufanya uhaini.

Kuhusiana na nukta hii, hivi karibuni duru za habari ziliarifu kuwa, wakati Bin Nayef alipokamatwa, alitandikwa vibaya sana  na sasa hawezi kutembea tena bila msaada. Mtandao wa Twitter unaofichua habari za ndani ya utawala wa kifalme wa Saudia wa al A'hdul Jadid umeripoti kuwa, Bin Nayef anateswa kwa maelekezo na amri ya moja kwa moja ya Bin Salman.

Baadhi ya mitandao ya kijamii imefichua kuwa, hali ya Bin Nayef ni mbaya kiasi kwamba yamkini akafariki dunia wakati wowote.

Kuhusiana na hili, mawakili wake wamewahi kutangaza kuwa, hivi sasa Bin Nayef anashikiliwa katika jela isiyojulikana na hana ruhusa ya kuonana na daktari wala kuwa na uhusiano na yeyote yule nje ya jela.

Jamal Khashoggi

Aidha tovuti ya 'Saudi Leaks" hivi karibuni ilifichua kuwa Mohammad bin Salman ameamua kutekeleza oparesheni ya  'mauaji ya kimya kimya' dhidi ya Bin Nayef ambaye ni kati ya wapinzani wake wakuu. Kwa kumtesa hadi afe, Bin Salman anataraji kuwa hatalaumiwa iwapo Bin Nayef atafariki kwani itadaiwa kilikuwa kifo cha kawaida.

Kuuzuliwa Bin Nayef na mateso anayokumbana nayo gerezani  sambamaba na ukandamizaji na ukatili  ambao Bin Salman anatekeleza dhidi ya wapinzani wake, hasa mauaji yasiyo na kifani kwa kutumia msumeno dhidi ya mwandishi wa makala Msaudi Jamal Khashoggi mwezi Oktoba mwaka 2018, yote hayo yamefanyika kwa idhini ya Marekani na Wamagharibi. Madola hayo yanayodai kutetea haki za binadamu hayajachukua hatua zozote za maana dhidi ya Saudia kufuatia ukatili huo uliovuka mipaka wa Bin Salman.

Historia ya kisasa ya Saudia imejaa vitendo vya mauaji na ukatili, utumiaji mabavu na ukiukwaji wa haki za binadamu. Pamoja na hayo kipindi kichafu zaidi katika historia ya Saudia kilianza kushuhudiwa mwaka 2017 wakati Bin Salman alichukua nafasi ya mrithi wa kiti cha ufalme. Inaonekana kuwa baba yake amempa hata mamlaka ya mfalme na sasa kimsingi yeye ndiye mtawala mkuu wa Saudia. La kushangaza ni kuwa hadi sasa hakuna asasi yoyote ya kimataifa iliyochukua hatua za kivitendo za kukabiliana na jinai hizo za ukoo wa Al Saudi ambazo aghalabu ni dhidi ya watu wa kawaida wasio na hatia.

Tags