Jul 15, 2021 11:26 UTC
  • Harakati za ukombozi Palestina zailaani Imarati kwa kufungua ubalozi Tel Aviv

Harakati za ukombozi wa Palestina zimeilaani nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kufungua ubalozi huko Tel Aviv, wiki chache tu baada ya Israeli kuuwa zaidi ya Wapalestina 255 katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Ubalozi wa Emirati mjini Tel Aviv, ulifunguliwa Jumatano iliyopita wiki mbili baada ya uzinduzi wa ubalozi wa Israeli huko Abu Dhabi.

Taarifa iliyotolewa na harakati ya Hamas yenye makao yake Ukanda wa Gaza imesema kuwa, hatua ya Imarati (UAE) ni kielelezo cha kuendelezwa makosa makubwa yaliyofanya ya utawala wa Abu Dhabi dhidi ya Wapalestina na watu wote wa kanda hii ambao wanapinga kikamiilifu aina zote za uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa: "Hatua hiyo ya Imarati ni kielelezo cha kurudi nyuma kisiasa kwa dola la Imarati ambako sio tu kwamba kunafunika rasmi kwa uhalifu uliofanywa na adui wa Mzayuni dhidi ya watu wa Palestina, lakini pia kunaushajiisha utawala huo uendeleze uhalifu na sera zake za kibaguzi."

Hamas imesema, UAE na nchi zingine za Kiarabu zikizoanzisha uhusiano na Israeli hivi karibuni "zitagundua ukubwa na uzito wa uhalifu wao," na imezitaka kurekebisha njia hiyo mbaya na kukata mahusiano yao yote na Israel.

Wakati huo huo, Tarek Silmi, msemaji wa harakati ya Jihad Islami amesema watawala wa Imarati wamekimbilia kufungua ubalozi wao huko Tel Aviv katika kipindi ambacho Israel imezidisha uhalifu wa kukalia kwa mabavu ardhi ya a al-Quds, kubomoa nyumba za raia wa Palestina na kushambulia Msikiti wa Al-Aqsa.

Wakati huo huo, Chama cha Popular Front for the Liberation of Palestine (PFLP) kimesema Waarabu wanaoanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel ni wasaliti, na kuongeza kuwa, kuzinduliwa ubalozi wa UAE katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu ya Palestina kuna maana ya kuhama kutoka kwenye awamu ya "kuanzisha uhusiano na kuingia kwenye Uzayuni."

Septemba mwaka  2020 Imarati na Bahrain na baadaye Sudan zilitia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Israel katika sherehe rasmi iliyoandaliwa na rais wa zamani wa Merikani, Donald Trump katika Ikulu ya White. 

Tags