Jul 18, 2021 03:06 UTC
  • Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu yataka kukomeshwa hujuma dhidi ya Masjidul-Aqswa

Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu imeutaka Umma wa Kiislamu na watu huru duniani kuchukua hatua za kuzuia hujuma na mashambulio ya Wazayuni dhidi ya msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu.

Taarifa hiyo imetolewa na Sheikh Ali al-Qaradaghi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu baada ya wito uliotolewa na walowezi wa Kizayuni wa kuchochea kuendelezwa hujuma na mashambulio dhidi ya msikiti wa al-Aqswa.

Katika taarifa hiyo, Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu imewataka wananchi wote Palestina hususan wakazi wa mji wa Quds na viunga vyake kujitokeza na kuutetea msikiti huo mtakatifu.

Kabla ya hapo pia, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Haraakti ya Jihadul Islami ya Palestina pia zilikuwa zimewataka wananchi wa Palestina kuwa tayari kuutetea msikiti wa al-Aqswa.

 

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Hata hivyo kusimama kidete wananchi wa Palestina hadi sasa kumekwamisha njama na mipango yote michafu ya Wazayuni, zikiwemo njama zake za kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa Baytul-Muqaddas.

Uvamizi huo unakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Palestina na kuwatimua Wapalestina kutoka katika ardhi zao sanjari na kubomoa nyumba zao.

Tags