Jul 18, 2021 08:15 UTC
  • Wanaharakati wa Saudia kufanya maandamano ya kupinga serikali Siku ya Arafa

Wanaharakati wa Saudi Arabia wamepanga kufanya maandamano ya kitaifa dhidi ya utawala wa Al Saud Siku ya Arafa.

Maandamano hayo yatafanyika Jumatatu ya kesho katika Siku ya Arafa, yaani tarehe 9 Mfunguo Tatu Dhulhija ambapo mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Makka husimama katika eneo la Arafa kwa ajili ya ibada maalumu ya siku hiyo.

Washiriki katika maandamano hayo watalaani utawala wa koo wa Aal Saud na kutoa wito wa kuwepo uhuru na vilevile kukomeshwa mporomoko wa kiuchumi katika nchi hiyo ya kifalme.

Mwanaharakati wa upinzaji wa Saudi Arabia mwenye makao yake nchini Marekani, Ali al-Ahmed amesema kwamba amepewa heshima kuwa afisa mawasiliano na vyombo vya habari wa maandamano hayo.

Siku ya Arafa ni siku takatifu katika kalenda ya Kiislamu, na siku ya pili ya ibada ya Hija. Siku inayofuata yaani tarehe 10 Dhulhija ni siku ya kwanza ya sikukuu ya Eid al-Adha.

Siku ya Arafa ya kila mwaka mahujaji hukusanyika kwenye Mlima Arafat, unaojulikana pia kama Jabal al-Rahma (Mlima wa Rehema), karibu na mji mtakatifu wa Makka, ambapo hufanya maombi maalumu, wakiomba msamaha wa Mwenyezi Mungu na rehma Zake.

Mlima Arafa

Ibada tukufu ya Hija ilianza rasmi juzi nchini Saudi Arabia chini ya usimamizi na sheria kali za kukabiliana na maambukizo ya virusi vya Corona huku idadi ya mahujaji ikiwa chache mno.

Saudi Arabia inalaumiwa sana na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kwa hostoria yake mbaya ya kuwakandamiza wanaharakati wa masuala ya kisiasa na haki za binadamu na kuwaua au kuwafunga jela wapinzani. 

Tags