Jul 22, 2021 11:30 UTC
  • Kufichuliwa engo mpya wa ushirikiano wa Marekani na kundi la Daesh nchini Afghanistan

Zamir Kabulov, mjumbe wa Rais wa Russia katika masuala ya Afghanistan amesema katika mkutano wa Valdai Discussion Club kwamba: Askari wa Marekani na waitifaki wake walikuwa na mawasiliano na ushirikiano na kundi la kigaidi la Daesh nchini Afghanistan.

Kabulov sambamba na kubainisha juu ya kuweko ushirikiano kama huu huko nyuma baina ya muungano wa vikosi vya kigeni ukiongozwa na Marekani ameeleza kwamba: Tumepokea taarifa za kiintelijensia kutoka nchini Afghanistan ambazo zinathibitisha juu ya kuweko ushirikiano wa majeshi ya Marekani na waitifaki wake na kundi la kigaidi la Daesh huko nchini Afghanistan.

Mjumbe wa Rais wa Russia katika  masuala ya Afghanistan ameashiria mfano mmoja wa kuzingirwa kundi kubwa la magaidi wa Daesh kaskazini mwa Afghanistan na kusema kuwa: Magaidi hao walihamishwa kwa helikopta zisizo na utambulisho na kupelekwa katika kambi ya kijeshi ya Bagram na kisha baadaye wakasambazwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Aidha anaeleza kwamba, matukio madogo kama haya ni mengi na mtu anapofanya uchunguzi wa jumla wa matukio yote haya anaweza kufikia natija jumla.

Madhumuni ya afisa huyo wa Russia ya kufikia natija jumla ni kwamba, Marekani ilikuwa ikishirikiana na Daesh na kulisaidia kundi hilo la kigaidi huko nchini Afghanistan kwa sura iliyoratibiwa na katika fremu ya mpango jumla.

Zamir Kabulov, Mjumbe wa Rais wa Russia katika  masuala ya Afghanistan

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, uwepo wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan ulikwenda sambamba na kuibuka na kisha kuenea harakati za kundi la kigaidi la Daesh nchini humo. Serikali ya Russia imeonya mara kadhaa kwamba, kundi la kigaidi la Daesh limo mbioni kueneza harakati zake nchini Afghanistan lengo likiwa ni kufika katika eneo la Asia ya Kati na kulitumbukiza eneo hilo katika kinamasi cha vurugu na machafuko.

Kadhalika Russia ilitoa indhari kuhusiana na kuenea uwepo wa kundi la kigaidi la Daesh nchini Afghanistan; na ikiwa na lengo la kuzuia harakati za kundi hilo dhidi ya waitifaki wake katika Jumuiya ya Mkataba wa Usalama wa Pamoja (CSTO) ilichukua hatua kadhaa ambapo kuimarisha vituo vya kijeshi vya nchi hiyo katika nchi za Tajikistan na Kyrgyzstan ni miongoni mwa hatua hizo. Warusi wanaamini kuwa, Wamarekani na waitifaki wakiwa na nia ya kufuatilia malengo yao nchini Afghanistan wamekuwa wakitoa misaada ya kilojistiki na kisilaha kwa kundi la kigaidi la Daesh nchini Afghanistan.

Kwa kuzingatia tishio la usalama linalotokana na hatua hii, Moscow inataka kuwekwa wazi na kufichukuliwa engo na wigo wa hatua hii na kusitishwa mara moja mwenendo huu. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia kabla ya hapo ilikuwa imetangaza kuwa, maeneo ya kaskazini mwa Afghanistan yamegeuka na kuwa maficho ya wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh.

 Kujiimarisha kundi la kigaidi la Daesh nchini Afghanistan kwa kuzingatia utendaji wa Marekani katika uga wa kuunga mkono uwepo wa kundi hilo nchini Afghanistan na hata misaada yake kwa magaidi hao ya kuingia na kupelekwa katika maeneo maalumu ni jambo linalopata umuhimu. Maria Zakharova, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia anasema kuhusiana na kadhia hii kwamba: Kwa kuzingatia taarifa zilizopo ambazo ni za kuaminika, inawezekana kusisitiza kabisa juu ya kuwepo himaya na misaada ya Marekani na Muungano wa Kijeshi wa NATO kwa wanachamna wa Daesh nchini Afghanistan, ambapo misaada hii inajumuisha usafiri na uchukuzi unaofanywa na helikopta za kijeshi zisizo na utambulisho na kupatiwa magaidi hao silaha hatari.

Wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan

Marekani daima imekuwa ikilitumia kundi la kigaidi la Daesh kama wenzo wake dhidi ya maadui wake wa kieneo na kimataifa ikiwemo Iran, Russia na China; na hata kuliimarisha kundi la Daesh nchini Afghanistan hususan katika ukanda wa jirani na mataifa ya Asia ya Kati kama Tajikistan na Uzibekistan kunafanyika kwa shabaha ya kuishinikiza Russia, China  na kadhalika.

Nouzar Shafi’i, mweledi na mtaalamu wa masuala ya kimataifa sambamba na kusisitiza kwamba, kwa upande wa kijamii kundi la Daesh halina nafasi yoyote nchini Afghanistan na kuongeza kuwa, Marekani inafanya njama ikilitumia kundi hilo ili kuitoa China nchini Afghanistan na hivyo kutoa pigo la ndani kwa mshindani na hasimu wake huyo.

Licha ya Marekani kutuma majeshi yake nchini Afghanistan miaka 20 iliyopita kwa nara na kaulimbiu ya kwenda kupambana na ugaidi, lakini filihali Afghanistan iko katika kilele cha nchi zinazotaabika kwa mashambulio ya kigaidi. Hadi sasa Marekani imeshaondoa asilimia 95 ya askari wake kutoka Afghanistan na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kundi la Taliban limekuwa na harakati zaidi na limedhibiti maeneo mapya nchini humo. Wakati huo huo, kuzidi kuzorota hali ya usalama nchini Afghanistan kumepelekea kushadidi operesheni za kigaidi za kundi la Daesh. Hadi sasa kundi la Daesh limetekeleza mashambulio na milipuko kadhaa na kusababisha mamia ya wananchi wa Afghanistan kuaga dunia.

Tags