Jul 24, 2021 11:55 UTC
  • Hizbullah Iraq: Wanajeshi wa Marekani wanapaswa kuondoka kwenye ardhi ya Iraq, la sivyo watashambuliwa

Afisa usalama wa Batalioni ya Hizbullah nchini Iraq ametangaza kuwa, iwapo wanajeshi wa Marekani hawataondoka nchini Iraq, makundi ya mapambano yataendelea kutekeleza mashambulizi dhidi ya wavamizi hao.

Abu Ali al Askari ambaye alikuwa akizungumzia mazungumzo ya kistratijia yanayoendelea baina ya Baghdad na Washington amesema kuwa, wanasiasa wa serikali ya Baghdad wanapaswa kutoa ufafanuzi kwa taifa la Iraq kuhusu falsafa ya mchezo wa kuigiza unaofanyika kupitia kalibu ya mazungumzo hayo.

Vievile Kamati ya Uratibu ya Makundi ya Mapambano ya Iraq mapema leo imetoa taarifa ikisisitiza ulazima wa kuondoka wanajeshi wote wa kigeni katika ardhi ya Iraq na kutangaza kuwa, jukumu kuu na kikosi cha anga cha Marekani nchini Iraq ni kulinda usalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kufanya ujasusi dhidi ya makundi ya mapambano; hivyo wanapaswa kuondoka kikamilifu katika ardhi yote ya Iraq. 

Matamshi hayo yametolewa wakati huu ambapo Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi anatarajiwa kukutana na Rais Joe Biden wa Marekani siku ya Jumatatu ijayo ili kujadili suala kukamilishwa mazungumzo ya kistratijia baina na Baghdad na Washington. 

Bunge la Iraq

Tarehe 5 Januari mwaka jana Bunge la Iraq lilipasisha azimio la kufukuzwa vikosi vya majeshi ya nchi za kigeni hususan Marekani katika ardhi ya Iraq. Uamuzi huo wa Bunge la Iraq ulichukuliwa baada ya jeshi la Marekani kufanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Abu Mahdi al-Muhandis aliyekuwa afisa wa wapiganaji wa kujitolea wa harakati ya al Hashdul Shaabi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad.

Luteni Jenerali Qassim Soleimani alikuwa safarini nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa waziri mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo.   

Tags