Jul 25, 2021 01:19 UTC
  • Mpango wa kuanzisha utawala wa ndani Syria, njama ya wapinzani wa serikali ya Damascus

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetangaza kuwa, kile kinachoitwa "serikali ya mamkala ya kujiendeshea mambo yake" ni mpango wa kutaka kuiodhoofisha nchi hiyo.

Mwaka 2011 Syria iliingia katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi yaliyoanzishwa na kufadhiliwa na nchi za Kiarabu na Kimagharibi. Makundi hayo yanaundwa na raia wa zaidi ya nchi 100 na wamekuwa wakipewa himaya na misaada na nchi za kigeni. Lengo kuu la vita hivyo lilikuwa kuiondoa madarakani serikali halali. Hata hivyo baada ya muongo mmoja sasa, ndoto hiyo haijatimia, na serikali ya Damascus inadhibiti maeneo mengi ya Syria isipokuwa sehemu ndogo tu ya ardhi ya nchi hiyo huko Idlib na kaskazini mwa Syria ambayo inadhibitiwa na makundi ya kigaidi yanayolindwa na kupewa himaya na majeshi ya Marekani. Mwezi Mei mwaka huu pia kulifanyika uchaguzi wa rais nchini humo na Bashar Assad alishinda kinyang'anyiro hicho kwa kupata asilimia 95 ya kura za wananchi.

Kwa kutilia maanani kwamba, serikali ya Syria imepata ushindi mkubwa katika medani ya vita, sasa wapinzani wake wameamua kutumia ulingo wa siasa kwa ajili ya kutoa dharuba na pigo kwa serikali ya Damascus. Moja kati ya silaha za kisiasa zinazotumiwa na wapinzani wa serikali ya Syria ni mpango wa kuanzisha utawala wa ndani katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo yakiwemo yale ya kaskazini na kaskazini mashariki. Kwa sasa waasi wa Kikurdi wanashikilia maeneo ya kaskazini mwa Syria wakiwa na lengo ya kuanzisha utawala wa ndani chini ya himaya na uungaji mkono wa Marekani. Waasi hao wa Syria wanataka kuanzisha utawala wa ndani kama ule wa Kurdistan huko kaskazini mwa Iraq. Mazloum Abdi ambaye ni miongoni mwa makamanda wa wanamgambo wa kundi la waasi wa Kikurdi la SDF amekuwa akisema mara kwa mara kwamba, hali ya Syria haiwezi kuwa kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2011 na kwamba Wakurdi wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi katika serikali.  

Mazloum Abdi

Ili kutimiza lengo lao, waasi hao wa Kikurdi wametwaa visima vya mafuta vya kaskazini mashariki mwa Syria na wanafanya biashara ya magendo ya bidhaa hiyo kwa ajili ya kudhamini vyanzo vya fedha vya utawala wa ndani katika eneo hilo wakisaidiwa na Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya. Katika uwanja huo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa eti mamlaka ya ndani ya Wakurdi wa Syria katika Ikulu ya Élysée. Berivan Khalid ambaye ni miongoni mwa maafisa wa “utawala wa ndani” huko kaskazini mwa Syria ambaye pia alishikiriki katika mazungumzo hayo amesema kuwa, kikao cha Paris kilijikita kwenye himaya na uungaji mkono wa Ufaransa kwa suala la kutambuliwa rasmi kimataifa utawala wa ndani wa Wakurdi nchini Syria.

Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Syria imetangaza kuwa, makundi yanayotaka kuunda “mamlaka ya ndani” katika eneo la kaskazini mashariki yamekuwa yakifanya safari za mara kwa mara katika baadhi ya nchi za Magharibi ili kuuza mpango huo wa kujitenga na Syria.

Nukta muhimu ya kutiliwa mkazo hapa ni kwamba, lengo kuu la mpango huo ni kudhoofisha utawala wa Syria. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, mpango wa kuanzisha mamlaka ya ndani ni njama inayofanyika dhidi ya taifa la Syria kwa uratibu na himaya ya nchi za Magharibi na baadhi ya madola ya Kiarabu. Baada ya kushindwa kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria kwa njia ya vita katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, sasa madola hayo yameamua kutumia njama ya kuanzisha “mamlaka ya utawala wa ndani” kuidhoofisha nchi hiyo.

Jeshi vamizi la Marekani katika ardhi ya Syria

Kudhoofishwa serikali kuu ya Syria kutakuwa na manufaa zaidi kwa utawala haramu wa Israel. Hi ni kwa sababu kwa pande mmoja Syria inapakana na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel na ina mzozo na utawala huo kuhusu ardhi ya Golan inayokaliwa kwa mabavu. Katika upande mwingine Syria ni miongoni nchi za kambi ya mapambano dhidi ya mabeberu; hivyo kuidhoofisha nchi hiyo ni kutoa pigo kwa kambi hiyo ya mapambano.

Wakati huo huo kuanzishwa mamlaka ya utawala wa ndani au mfumo wa federali huko kaskazini mashariki mwa Syria kutakuwa tishio kwa umoja wa ardhi ya nchi hiyo katika siku za usoni. Kwa msingi huo Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Syria inasisitiza kuwa, mpango huo wa waasi wa Kikurdi ni njama inayolenga kuigawa nchi hiyo kwa hiyama na uungaji mkono wa madola ya Magharibi hususan Marekani.  

Tags