Jul 25, 2021 01:21 UTC
  • HAMAS yalaani kuidhinishwa Israel kuwa mwanachama mtazamaji wa AU

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel kibali cha kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo.

Katika taarifa jana Jumamosi, HAMAS imesema uamuzi huo wa AU si tu utaupa uhalali utawala ghasibu wa Israel wa kuendelea kupora ardhi zaidi za Wapalestina, lakini pia utaushajiisha na kuupa nguvu utawala huo haramu za kuendelea na njama yake ya kutaka kufuta haki za Wapalestina.

HAMAS imesema kitendo cha Umoja wa Afrika kuuidhinisha utawala pandikizi wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji wa taasisi hiyo kubwa zaidi ya kibara ni sawa na kuubariki utawala huo uendeleze jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina.

Taarifa ya harakati hiyo ya muqawama imeyataka mataifa ya Afrika ambayo inasema yangali yamenasa kwenye minyororo ya ukoloni na ubaguzi, kuifukuza Israel katika AU, sambamba na kuiwekea vikwazo mpaka ikubali kufuata njia ya 'ukweli na haki.'

Nembo ya AU

Siku ya Alkhamisi, utawala haramu wa Israel ulitangaza kuwa umeidhinishwa kuwa mwanachama mtazamaji wa AU baada ya eti jitihada za kidiplomasia za karibu miongo miwili.

Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita, Shirikisho la Wanahabari wa Afrika (FAJ) liliutaka Umoja wa Afrika (AU) ulaani mienendo ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwashambulia wanahabari wa Palestina, sanjari na kuubebesha dhima kisheria utawala huo kwa jinai zake dhidi ya wanahabari hao kila leo.

 

 

Tags