Jul 25, 2021 02:58 UTC
  • Serikali ya Iraq yawatia mbaroni magaidi waliohusika na shambulio la umwagaji damu katika kiunga cha Sadr

Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi amesema, vyombo vya usalama vimewagundua na kuwatia mbaroni watu waliohusika na shambulio la kigaidi la mripuko wa bomu uliotokea kwenye kitongoji cha Sadr katika mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad.

Al Kadhimi ametoa tangazo hilo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa twitter na kueleza: "Machozi na maunguliko ya nyoyo za familia za mashahidi wa kitongoji cha Sadr vimetuongoza kwenye utekelezaji wa operesheni ya kuwatia nguvuni wanachama wote wa mtandao wa kigaidi, waliopanga na kutekeleza shambulio dhidi ya soko la Al Wahilat katika kitongoji cha Sadr."

Waziri Mkuu wa Iraq ameongeza kuwa, watu hao watakuwa funzo la ibra na mazingatio kwa kila mhalifu mbele ya taifa na sheria.

Athari za shambulio la kigaidi nchini Iraq

Ripoti kutoka Baghdad zinasema, baada ya tangazo hilo alilotoa hapo jana, Mustafa al Kadhimi alionana pia na familia za wahanga wa shambulio la kigaidi la mripuko wa bomu uliotokea katika kitongoji cha Sadr.

Watu 30 waliuawa na wengine 50 walijeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea Jumatatu iliyopita katika soko la Al Wahilat lililoko kwenye kitongoji cha Sadr mashariki ya mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) lilitangaza kuhusika na shambulio hilo.../

Tags