Jul 25, 2021 07:30 UTC
  • Katibu Mkuu wa GCC atoa porojo jingine jipya dhidi ya Iran ili kuzifurahisha tawala za Saudia na Imarati

Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi GCC, katika kile kinachoonekana kama nia ya kuzifurahisha tawala za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ameituhumu tena Iran kuwa inavuruga uthabiti na kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiarabu.

Nayef Falah Mubarak Al-Hajraf amerudia tena tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kudai kwamba, Iran inalenga kuvuruga uthabiti wa eneo na kuingilia mambo ya ndani ya nchi za Kiarabu.

Katika mwendelezo wa porojo lake hilo, Al-Hajraf amesema, haipasi mazungumzo ya nyuklia ya Vienna yahusiane na kutekelezwa upya makubaliano hayo ya JCPOA pekee.

Kwa mashinikizo ya Imarati na Saudia, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa GCC nao pia hivi karibuni walizusha madai kadhaa yasiyo na msingi dhidi ya Iran na kudai kwamba, nchi wanachama wa baraza hilo nazo pia inapasa zishirikishwe katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Saeed Khatibzadeh amejibu madai na tuhuma hizo kwa kusema, sera za baadhi ya nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ni za kiundumakuwili, kutokana na upande mmoja kudai kwamba zinataka kuboresha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kwa upande mwingine zinazusha madai yasiyo na msingi dhidi yake; na akasisitiza kuwa, GCC limekuwa mateka wa uchu wa siasa na sera zilizofeli za nchi chache zenye makelele mengi ndani ya baraza hilo.../