Jul 25, 2021 07:48 UTC
  • New York Times: Marekani haina nia ya kuwaondoa askari wake Iraq

Gazeti la New York Times limeeleza katika ripoti kuhusiana na safari anayotazamia kufanya Waziri Mkuu wa Iraq mjini Washington hivi karibuni, kwamba Marekani haina nia ya kuwaondoa askari wake walioko nchini humo.

Katika ripoti yake hiyo, New York Times limeandika kuwa, waziri mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi ataelekea Washington akiwa na azma ya kuwasilisha takwa la kuondolewa askari wa Marekani walioko Iraq, katika hali ambayo maafisa wa Marekani wametangaza kuwa askari 2,500 wa nchi hiyo walioko Iraq hawataondoka nchini humo, isipokuwa kitadkachofanyika ni kubadilishwa kimaandishi tu wajibu na majukumu yao.

Waziri Mkuu wa Iraq anatazamiwa kufanya safari ya pili kuelekea mjini Washington kesho Jumatatu huku mpango uliopitishwa na bunge la nchi yake wa kutaka askari wa Marekani waondoke katika ardhi ya nchi hiyo ukiwa bado haujatekelezwa hadi sasa.

Mustafa al Kadhimi

Baada ya shambulio la kigaidi lililofanywa Januari 7,2020 na jeshi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq la kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Suleimani, aliyekuwa kamanda wa kikosi cha quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq al Hashdu-Sha'abi pamoja na wenzao kadhaa walioandamana nao, bunge la Iraq lilipasisha mpango wa kutaka askari vamizi wa Marekani waondoke katika ardhi ya nchi hiyo. Hata hivyo licha ya kupita zaidi ya mwaka mmoja tangu kupitishwa mpango huo, Marekani haijaheshimu agizo hilo la bunge na takwa la wananchi wa Iraq na hadi sasa inatoa kila aina ya visingizio ili iendelee kubaki kijeshi nchini humo.../