Jul 26, 2021 07:53 UTC
  • Safari ya Al Kadhimi mjini Washington sambamba na duru ya nne ya mazungumzo baina ya Iraq na Marekani

Duru ya nne ya mazungumzo kati ya Marekani na Iraq ilianza siku ya Ijumaa ya tarehe 23 Julai mjini Washington, Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hussein na Qassem Al Aa'raji, Mshauri wa Usalama wa Taifa ndio wanaoiwakilisha nchi yao katika mazungumzo hayo.

Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa Al Kadhimi, ambaye jana Jumapili alielekea mjini Washington, leo anatazamiwa kukutana na Rais wa Marekani Joe Biden; na mazungumzo baina ya nchi mbili yataendelea kwa kuhudhuriwa na viongozi hao.

Rais Joe Biden wa Marekani (kulia) na Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa Al Kadhimi 

Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Baghdad na Washington ilifanyika mwezi Juni 2020, duru ya pili ikafanyika Septemba mwaka huo na duru ya tatu baina ya pande mbili ilifanyika Aprili mwaka huu. Mazungumzo ya sasa ni ya duru ya nne ya mazungumzo baina ya pande hizo mbili katika kipindi cha mwaka mmoja sasa. Sababu kuu ya kuanzishwa mazungumzo hayo ni kitendo cha kigaidi kilichofanywa na Marekani tarehe 3 Januari, 2020 ndani ya ardhi ya Iraq, cha kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Suleimani, kamanda wa wakati huo wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq, Al Hashdu-Sha'abi. Ajenda nyingine ya mazungumzo baina ya pande mbili ni kuhusu kuondoka askari wa jeshi la Marekani katika ardhi ya Iraq, kwa sababu mnamo tarehe 5 Januari 2020, Bunge la Iraq lilipitisha mpango unaowataka askari wa kigeni waondoke nchini humo.

Bunge la Iraq

Mwafaka uliopatikana hadi sasa katika duru tatu za mazungumzo ni pande zote mbili kuafiki askari wa Marekani waondoke nchini Iraq. Lakini pamoja na hayo, na licha ya maafisa wa Baghdad na Washington kusisitiza juu ya kuondoka askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq, ushahidi na kauli zinazotolewa zinaonyesha kuwa, serikali ya Iraq haipendelei kuona askari vamizi wa Marekani wanaondoka nchini humo; na hilo ndilo takwa la Washington pia. Na kwa sababu hiyo, serikali ya Iraq inatumia kisingizio cha ulazima wa kupatiwa mafunzo ya kijeshi na msaada wa kiintelijensia, ili kuhakikisha baadhi ya askari wa Marekani wanabakia nchini humo.

Kabla ya kuelekea Washington hapo jana, Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa Al Kadhmi alisema, hakuna haja yoyote ya vikosi vya majeshi ya kigeni kuendelea kuwepo katika ardhi ya Iraq. Lakini wakati huohuo akaeleza kwamba, Iraq ingali inahitaji kupatiwa mafunzo na Marekani na msaada wa kukusanya taarifa za kiintelijensia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hussein, naye pia alitangaza siku ya Ijumaa, katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na waziri mwenzake wa Marekani mjini Washington kwamba, "ili kuweza kukabiliana na DEASH (ISIS) tunahitaji muungano wa kimataifa na ushirikiano wake katika ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia." Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq akaongezea kwa kusema: "vikosi vyetu vya usalama vingali vinahitaji mipango ya mafunzo na zana za kijeshi za Marekani."

Askari vamizi wa Marekani katika ardhi ya Iraq

Kumetolewa kauli na maoni mbalimbali kuhusu askari wa jeshi la Marekani kuondoka nchini Iraq, lakini tathmini na ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa, upo uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya askari hao kuondoka nchini humo hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Kuna matarajio kwamba katika mazungumzo yao watakayofanya leo Ikulu ya White House, Biden na Al Kadhimi watatangaza ratiba kuhusu tarehe hasa ya kuondoka askari hao na inawezekana ikawa ni hiyo hiyo ya mwishoni mwa mwaka huu. Qassem al Aa'raji, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq, ambaye hivi sasa yuko kwenye mazungumzo ya Washington alitangaza siku ya Ijumaa kwamba: "Sisi tumewasisitizia Wamarekani kuwa Iraq haihitaji kuwepo katika ardhi yake askari wowote wa kigeni wa kupigana vita. Tarehe 31 Desemba, 2021 itakuwa ni siku yenye ladha maalum."

Tunachoweza kusema hapa ni kwamba "kuwepo kiushauri" ni msamiati wa fumbo ambao maafisa wa Marekani na Iraq wamepanga kuutumia ili kuwabakisha askari wa Marekani nchini Iraq na kupuuza mpango uliopitishwa Januari 5, 2020 na bunge la nchi hiyo kutaka majeshi yote ya kigeni yaondoke nchini humo. Mustafa Al Kadhimi, waungaji mkono wake na makundi yaliyo karibu naye wanajaribu kuutumia mwanya wa kuainishwa ratiba ya muda maalum wa askari wa vitani wa Marekani kuondoka nchini Iraq, ili kuweza kufanikisha malengo yao ya kiuchaguzi, ambao umepangwa kufanyika tarehe 10 Oktoba. Wakati huohuo, baadhi ya wanajeshi wa Marekani watabakia huko Iraq kwa kisingizio cha utoaji mafunzo na kutoa misaada ya kiinteljensia ili kudumisha uungaji mkono wa Marekani kwa serikali ya sasa ya nchi hiyo pamoja na waungaji mkono wake.../

Tags