Jul 28, 2021 08:23 UTC
  • Radiamali tofauti za maafisa na makundi ya Iraq kuhusu taarifa ya pamoja ya al-Kadhimi na Biden

Rais Joe Biden wa Marekani na Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq wametoa taarifa mwishoni mwa duru ya nne ya mazungumzo ya kistratijia nya nchi mbili ambapo wamesema kuwa wameafikiana juu ya kufikia kikomo uwepo wa askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kumalizika kipindi hicho nafasi ya askari wa Marekani huko Iraq itabadilika na kuwa ya kutoa mafunzo na habari za kijeshi tu.

Mapatano hayo ya Biden na al-Kadhimi yamepelekea kutolewa radiamali tofauti nchini Iraq ambapo baadhi ya makundi yameyakaribisha mapatano hayo na mengine kuyapiga kwa hoja kuwa hayajakuwa na mabadiliko yoyote ya msingi katika kuondolewa askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq bali ni mabadiliko ya kidhahiri tu ambayo hayana maana yoyote.

Rais Barham Salih wa Iraq na Mohammed al-Halbousi, Spika wa Bunge la nchi hiyo wamesifu mapatano hayo ya Biden na al-Kadhimi wakiyataja kuwa ni mafanikio makubwa ya kidiploamsia na kisiasa. Muungano wa al-Fat'h unaoongozwa na Hadi al-Amiri pia umeunga mkono mapatano hayo na kusema ni hatua chanya kwa ajili ya kufikia utawala kamili wa taifa la Iraq. Muqtada Sadr, Kiongozi wa Mrengo wa Sadr pia ameunga mkono mapatano hayo na kumshukuru al-Kadhimi kwa kuyafanikisha.

Rais Joe Biden wa Marekani (kushoto) na Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq

Hata kama pande hizo zimeunga mkono mapatano hayo lakini baadhi ya tofauti zinaonekana wazi katika misimamo yao. Msimamo wa Salih na al-Halbousi wa kuunga mkono mapatano hayo na kuyataja kuwa ni mafanikio makubwa ya kisiasa na kidiplomasia ya al-Kadhimi unachukuliwa kuwa ni wa kisiasa na uanaolenga kuimarisha nafasi yake katika uchaguzi ujao wa bunge ambao umepangwa kufanyika tarehe 10 Oktoba. Hii ni katika hali ambayo Muungano wa al-Fat'h na Sadr imeyataja mapatano hayo kuwa hatua inayoelekea katika kuimarisha utawala wa kitaifa wa Iraq na kuwa tokea sasa Wairaki wanataraji kuwa askari wote wa Marekani wataondolewa katika nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa maneno mengine ni kwamba mirengo ya al-Fat'h na Sadr inataka askari wote wa Marekani wakiwemo washauri wa kijeshi waondoke Iraq na kwamba mapatano ya Biden na al-Kadhimi yataandaa hatua ya baadaye ya kufikiwa lengo hilo.

Msimamo mwingine ni kutoka kundi la Harakati ya an-Nujabaa ya Iraq ambayo inaamini kuwa hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea katika suala zima la uwepo wa askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq. Akifafanua msimamo huo katika mahojiano na televisheni ya al-Mayadeen, Nasr as-Shammari, Msemaji wa Harakati ya an-Nujabaa amesema kwamba Iraq haihitajii askari wa Marekani na kwamba silaha zake zitawalenga askari hao kwa anwani yoyote ile. Amesema Wamarekani wamewahadaa Wairaki kwa kubadilisha na kuwapa askari wake anwani tofauti, na kwamba hilo halitabadilisha mtazamo wa an-Nujabaa kuhusu askari hao vamizi ambao sasa wanadaikuwa kuwa ni washauri wa kijeshi.

Askari vamizi wa Marekani nchini Iraq

Baadhi ya wachambuzi wa mambo licha ya kukaribisha mapatano hayo lakini bado wana shaka na wasi wasi mkubwa kuhusu iwapo kweli mapatano hayo yatatekelezwa kivitendo. Kuhusu hilo, Muhammad as-Sabai, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Iraq anasema, mapatano haya mapya hayana maana kwamba pande mbili hizi zina nia njema kuhusu kuondoka askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq.

Kwa kutilia maanani radiamali hizo na pia misimamo ya serikali za Marekani na Iraq, ni wazi kuwa hakuna mabadiliko yoyote muhimu ambayo yametokea kuhusu suala zima la kuondolewa askari wa Marekani huko Iraq kwa sababu hakuna hata idadi kamili ya askari wa Marekani wanaosemekana kuwa wataendelea kusalia Iraq kama washauri wa kijeshi. Wakati huo huo kungali kuna shaka kubwa na mambo mengi yasiyoeleweka vizuri kuhusiana na nafasi ya ushauri wa kijeshi wa askari hao. Isitoshe, hakuna miongozo wala mkakati wowote uliowekwa wazi kwa ajili ya kuondoka askari hao vamizi katika ardhi ya Iraq.

Tags