Jul 30, 2021 02:20 UTC
  • Maroketi mawili yapiga karibu na ubalozi wa Marekani, Baghdad

Ripoti zinasema kuwa maroketi mawili yamepiga eneo la karibu na ubalozi wa Marekani mjini Baghdad katika eneo lenye ulinzi mkubwa la Green Zone.

Vyombo vya usalama vya Iraq vimetangaza kuwa, maroketi hayo mawili yalikuwa aina ya Katyusha na kwamba yamelenga eneo la kandokando ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad. Ripoti ya vyombo vya usalama vya Iraq imesema kuwa, ngao wa kujikinga na makombora ya Marekani, C-RAM, haikuweza kuzua maroketi hayo na kwamba vipande vya silaha hizo vimepiga magari kadhaa na nyumba moja. 

Hilo ni shambulizi la kwanza la aina yake tangu baada ya kumalizika duru ya nne ya mazungumzo ya kistratijia baina ya Marekani na Iraq. 

Baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika siku chache zilizopita huko White House baina ya Rais Joe Biden wa Marekani na Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi, makundi ya mapambano ya Iraq yalitahadharisha kuwa, msimamo wao wa kupinga uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya Iraq uko palepale na kwamba yataendelea kuwa tayari hadi pale wanajeshi wote wa Marekani watakapoondoka katika ardhi ya Iraq.

Biden na al-Kadhim

 

Mustafa al Kadhimi na Biden wamekubaliana kwamba wanajeshi wa Marekani wataondoka katika ardhi ya Iraq hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu. 

Taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo ilisema, idadi ndogo ya askari wa Marekani itaendelea kuwepo nchini Iraq kwa ajili eti ya kutoa mafunzo na ushauri wa kijeshi.

Makubaliano hayo yamepingwa na makundi ya mapambano ya Iraq yanayosisitiza kuwa, wanajeshi wote wa Marekani wanapaswa kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo kwa mujibu wa agizo la Bunge la Iraq.    

Tags