Jul 30, 2021 08:36 UTC
  • Fursa na changamoto zilizoko mbele ya Najib Mikati

Kufuatia Sad Hariri, Kiongozi wa Chama cha Mustakbal kushindwa kuunda serikali mpya ya Lebanon hata baada ya kupita miezi 9 tokea apewe jukumu hilo, kutokana na kushikilia misimamo yake na kupuuza uwezo wa Rais Michel Aoun, Jumatatu alasiri, Rais Aoun alimpa Najib Mikati ambaye aliungwa mkono kwa kura 72 kati ya kura zote 120 za wabunge wa Lebanon, fursa ya kuunda serikali mpya ya nchi hiyo.

Jumanne makundi tofauti ya bunge yalimtaka Mikati aanzishe haraka juhudi za kuunda serikali ili kutuliza hali ya mambo nchini na kutowafanya wananchi waendelee kukata tamaa kuhusiana na mustkbali wa nchi yao. Katika matamshi yake ya kwanza baada ya kuteuliwa kuunda serikali, Najib Mikati amesema amepewa ahadi na baadhi ya nchi za kigeni kuwa zitamuunga mkono katika jitihada zake za kubuni serikali hiyo.

Ameashiria kwa njia isiyo ya moja kwa moja ahadi zilizotolewa na Ufaransa na vile vile Umoja wa Ulaya kuhusu suala hilo na kumtaka aunde serikali mpya ya Lebanon haraka iwezekanavyo. Inaonekana kuwa Marekani na Saudi Arabia pia zinataka serikali mpya ibuniwe haraka huko Lebanon ili kudhamini maslahi yao katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Bunge la Lebanon lililompa Mikati fursa nyingine ya kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo

Ni wazi kuwa vibaraka wa nchi hizo huko Lebanon kama Chama cha Vikosi vya Lebanon kinachoongozwa na Samir Ja'ja wanaendelea kupiga ngoma ya upinzani na lengo lao kuu ni kuifanya Lebanon isiwe na uthabiti wa kudumu ili kuitishwe uchaguzi wa mapema ambao umepangwa kufanyika mwaka ujao. Kwa vyovyote vile mazingira ya sasa ya Lebanon ni mazuri kwa ajili ya kuundwa serikali mpya.

Katika uapnde wa pili, ni wazi kuwa Najib Mikati ambaye ni mfanyabiashara na mwanasiasa mkongwe wa Lebanon hangekubali jukumu la kuunda serikali mpya kama angejua mazingira hayamruhusu kufanya hivyo. Ana uzoefu wa kuwa Waziri Mkuu wa Lebanon katika miaka ya 2005 hadi 2011 na kwa kawaida huwa haingii katika uwanja wa kisiasa akiwa na misimamo ya kitoto kama alivyofanya Sad Hariri karibuni.

Kikao chake cha ana kwa ana na bila wapatanishi na Gebran Bassil, kiongozi wa Chama cha Harakati Huru ya Uzalendo ya Lebanon baada ya kupewa jukumu la kuunda serikali ni thibitisho la wazi kuhusu suala hilo. Hii ni katika hali ambayo Sad Hariri alikuwa na uadui mkubwa na chama hicho na hasa na Gebran Bassil mwenyewe.

Kwa maelezo hayo, ushahidi na dalili zilizopo zinaonyesha kuwa Najib Mikati atafanikiwa kubuni serikali katika kipindi kifupi na hasa ikitiliwa maanani kwamba Mfuko wa Kimataifa wa Fedha tayari umeipa Lebanon mkopo wa dola milioni 860 na kutangaza kuwa ifikapo tarehe 4 Agosti ijayo utandaa mkutano wa kimataifa kwa ajili ya kuchangisha pesa za kuisadia Lebanon. Tayari Mikati ametangaza mipango ya kunufaika na mkutano huo pamoja na ahadi zilizotolewa kimataifa kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo.

Rais Michel Aoun wa Lebanon

Ni kwa msingi huo ndipo akawa na mataumaini makubwa kwamba atafanikiwa katika jukumu lake la kuunda serikali mpya ya Lebanon. Pamoja na hayo kuwepo kwa mazingira hayo chanya ya kubuniwa serikali mpya hakuna maana kwamba kwa sasa kila kitu ni shwari na kwamba hakuna changamoto zinazomkabili nchini. Hii ni kwa kuwa Lebanon ingali inakabiliwa na migogoro mikubwa ambayo iwapo haitatafutiwa ufumbuzi wa haraka, bila shaka itaongezeka zaidi na hivyo kumfanya Mikati asifanikiwe kuunda serikali ijayo. Ni wazi kuwa huenda Mikati akawa ni fursa ya mwisho ya kutatuliwa migogoro hiyo.

Kwa sasa Lebanon inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Thamani ya sarafu ya nchi hiyo imefikia kiwango cha chini kabisa mkabala na dola na bei ya nishati imeongezeka kwa kiwango cha kutisha suala ambalo bila shaka linaandaa uwanja wa kutokea nchini mlipuko wa kijamii wakati wowote. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba utawala ghasibu wa Israel unashirikiana na baadhi ya vibaraka wake wa kisiasa na wanaofungamana na nchi za Magharibi na baadhi ya tawala tegemezi za eneo nchini Lebanon kwa ajili ya kuchochea ghasia na machafuko, ili kufikia malengo yake na kuzuia kutatuliwa matatizo na kufikiwa umoja wa kitaifa katika nchi hiyo ya Kiarabu.