Aug 03, 2021 10:45 UTC
  • Naftali akiri kwamba Israel imeshindwa kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel amekiri kuwa sera za mtangulizi wake Benjamin Netanyahu kuhusiana na Iran zimefeli na akaeleza kwamba serikali iliyotangulia ya Tel Aviv ilipelekea makundi ya muqawama katika eneo kupata uwezo wa kujiwekea akiba ya maelfu ya makombora na maroketi.

Tovuti ya habari ya gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot imeripoti kuwa Naftali Bennett alieleza hayo katika kikao cha jana cha bunge la utawala wa Kizayuni (Knesset) kilichotawaliwa na malumbano makali na akabainisha kuwa, sera zilizoshindwa na kugonga mwamba za waziri mkuu aliyetangulia Benjamin Netanyahu katika kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeifanya serikali mpya ya Tel Aviv ilazimike kuongeza bajeti ya kijeshi, katika hali na mazingira magumu ya kiuchumi.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amekosoa pia hatua zilizochukuliwa na serikali ya Netanyahu katika kukabiliana na makundi ya muqawama ya Lebanon na Ukanda wa Gaza na akasema, Netanyahu alisababisha harakati ya muqawama ya Hizbullah kuwa na uwezo wa kuimarisha makombora yake yenye shabaha kali; na makombora hayo yanao uwezo wa kupiga shabaha yoyote katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).

Naftali Bennett amedai pia kwamba, "Iran inaendeleza kwa kasi mpango wake wa nyuklia na sisi tutakabiliana nao."

Kwa muda wa miaka kadhaa sasa baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zimekuwa zikiituhumu Iran kuwa eti inafuatilia malengo ya kjeshi katika mpango wake wa nyuklia, lakini Jamhuri ya Kiislamu imekanusha vikali madai hayo.

Iran inasisitiza kwamba, kwa kuwa ni moja ya nchi zilizosaini mkataba unaopiga marufuku uundaji na uenezaji silaha za nyuklia NPT, na mwanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, inayo haki ya kunufaika na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani.../