Aug 05, 2021 02:30 UTC
  • Njama za kukaririwa za kutaka kuidhihirisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman kuwa si eneo salama; sababu na malengo yake

Katika siku za hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari viliripoti habari ya kushambuiwa meli kadhaa katika pwani ya Imarati.

Shirika la habari la Associated Press limedai katika ripoti yake kwamba, manahodha wa meli zisizopungua nne walishindwa kudhibiti vyombo hivyo katika maji ya pwani mwa Imarati. Awali baadhi ya duru za habari pia zilikuwa zimeripoti kuwa, kumeshuhudiwa mlipuko katika meli moja karibu na bandari ya al Fujairah huko Imarati. 

Sambamba na habari hizo vyombo vya habari vya Kimagharibi na Kizayuni vilisambaza uvumi mwingi kwamba, wanajeshi wa Iran wameingia katika meli zinazopita katika maji ya Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Omani. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran, Saeed Khateebzadeh amekadhibisha madai na uvumi wa kuingia majeshi ya Iran katika meli zinazopita Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman na kutahadharisha kuhusu habari za uongo zinazosambazwa na vyombo vya habari vya Kimagharibi na Kizayuni. Alisema matukio ya kushambuliwa meli katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman yanatia shaka.

Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, matukio hayo yanayotiliwa shaka ya kushambuliwa meli katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Omani yanamfaidisha nani?

Nani anahusika na mashambulizi dhidi ya meli Ghuba ya Uajemi?

Kuna mitazamo miwili kuhusiana na swali hili: Kwanza ni kwamba matukio haya yanafanyika kwa makusudi kwa ajili ya kulidhihirisha eneo hilo kuwa ni tishio kwa meli za kibiashara na zile zinazobeba mafuta. Kwa hali hii inatupasa kusema kuwa, wapangaji wa njama hii wana malengo maalumu ya kuzusha hofu na wasiwasi kuhusiana na eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman. Njama hii inazishirikisha nchi kama Marekani, Uingereza, Saudi Arabia, Imarati, utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za kanda hii. Matamshi yaliyotolewa na Mkuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Joseph Dunford, katika uwanja huu yanapaswa kupewa mazingatio maalumu. Hivi karibuni alizungumza na waandishi habari kuhusu mpango wa Marekani wa kuanzisha eti muungano wa kudhamini uhuru wa safari za meli katika malango bahari ya Hormuz na Babul Mandab. Mkuu wa Majeshi ya Marekani pia alidai kuwa: Kuna uwezekano kwamba, wiki zijazo itaeleweka ni nchi gani zina azma ya kisiasa ya kuunga mkono mpango huo.

Mtazamo wa pili kuhusiana na njama hiyo ni kuzidisha mashinikizo ya kiusalama ya kiwango cha juu dhidi ya Iran kwa ajili ya kutimiza malengo mengine. Hapa kuna maudhui kuu mbili. Kwanza ni kuhusu hatima ya mazungumzo yaliyosimama ya nyuklia huko Vienna, na pili ni suala la kutaka kudhoofisha kambi ya muqawama na mapambano na uwepo wa majeshi ya Iran katika maeneo ya kistratijia ya Magharib mwa Asia.

Hivyo basi, si ajabu kwa Israel kuvuruga usalama wa Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman kwa shabaha ya kutimiza malengo hayo na kuifanya Iran ikabiliwe na changamoto bandia na za kubuni za kiusalama.

Shambulizi lililofanywa Ijumaa iliyopita na ndege isiyo na rubani dhidi ya meli ya Israel katika Bahari ya Oman linaimarisha zaidi mtazamo huu. Baada tu ya shambulizi hilo, na bila ya kutoa ushahidi wowote, maafisa wa Israel walijitokeza mbele ya vyombo vya habari na kuanza kuituhumu Iran kuwa ndiyo iliyotekeleza shambulizi hilo. Maafisa ho walitoa wito wa kutolewa jibu kali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Mchambuzi mashuhuri wa masuala ya Mashariki ya Kati, Abdel Bari Atwan alisema katika ripoti yake iliyochapishwa na gazeti la kikanda la al Rai al Arabi akijadili mikono ya nyuma ya pazia ya Marekani na Israel kwamba: “Shambulizi hili limefanyika sambamba na kusimamishwa mazungumzo ya kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na karibu na kipindi cha kuapishwa rais mpya wa Iran, Sayyid Ebrahim Raeisi.”

Abdel Bari Atwan

Mwezi Machi mwaka huu pia wakati wa homa ya uchaguzi wa Bunge la Israel katika utawala wa Benjamin Netanyahu, Abdel Bari Atwan aliandika tahariri kama hii akizungumzia uwezekano wa kufanyika mashambulizi dhidi ya meli zinazobeba mafuta katika mji ya Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman. Aliandika kuwa: Katika kipindi cha miaka miwili iyopita kundi maalumu la kikosi cha majini cha Israel limeshambulia meli 12 za kubeba mafuta za Iran.

Alaa kulli hal, ushahidi uliopo unazidisha shaka kuhusiana na njama hii ya kushambuliwa meli katika maji ya Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman. Hapana shaka kuwa, iwapo maafisa wa utawala wa Kizayuni watataka kuzidisha vita hivyo, basi watakuwa wamefanya kosa kubwa. Kwa sababu ochokozi huo unaweza kuwa na madhara makubwa sana kwa utawala huo, bwana wake, yaani Marekani na vibaraka wao wa Ghuba ya Uajemi.