Aug 05, 2021 07:48 UTC
  • Sana'a yakaribisha mazungumzo na Riyadh kwa ajili ya kuondoa mzingiro na kusitisha vita Yemen

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa Sana'a inakaribisha mazungumzo mapya baina yake na Riyadh ili kuondoa mzingiroa na kusitisha vita huko Yemen.

Hussein al Ezzi amesema jana usiku katika mahojiano na televisheni ya al Mayadeen kuwa, Riyadh na Sana'a zinapasa kuanzisha marhala mpya ya mazungumzo. Al Ezzi amesisitiza kuwa, Saudi Arabia inapasa kushirikiana na Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen huko Sana'a na pande mbili zinapasa kufanya juhud kubwa ili kuiondolea Yemen mzingiro unaoikabili na kusitisha vita nchini.

Al Ezzi amesema, si vyema kuona mamluki wa Saudia wakiendelea kukwamisha mchakato wa amani huko Yemen. Saudi Arabia huku ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa ziliivamia Yemen mwezi Machi mwaka 2015 na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, nchi kavu na anga. 

Hadi sasa Wayemeni zaidi ya elfu 16 wameuawa na makumi ya maelfu kujeruhiwa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi tangu Saudia na waitifaki wake waanzishe vita katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Uvamizi wa Saudia na waitifaki wake umebomoa na kuvuruga pakubwa miundo mbinu mbalimbali huko Yemen.