Aug 05, 2021 10:15 UTC
  • Saudi Arabia, jumba la mateso kwa wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kwa mara nyingine tena imeweka wazi rekodi mbaya na nyeusi ya utawala wa Saudi Arabia katika suala la haki za binadamu.

Amnesty International imetangaza kuwa, Saudi Arabia imezidisha ukandamizaji na kuwatesa wanaharakati wa kupigania haki za binadamu na haki za kiraia na kwamba idadi ya watu walionyongwa nchini humo pia imeongezeka sana katika kipindi cha miezi sita iliyopita. 

Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, lynn Maalouf amesema kuwa, baada tu ya kumalizika kipindi cha uenyekiti wa Saudi katika G20, maafisa wa serikali ya Riyadh walianza kutekeleza mienendo yao ya kikatili dhidi ya watu waliofanya ujasiri wa kutoa maoni huru au kukosoa utawala wa kifalme wa nchi hiyo na kwamba, wapinzani 9 wamenyongwa nchini humo katika mwezi Disemba mwaka jana pekee. Taarifa ya Amnesty International imesema watu wasiopungua 40 walinyongwa nchini Saudi Arabia katika kipindi cha baina ya Januari na Julai mwaka huu wa 2021 na kwamba kiwango hicho peke yake ni kikubwa zaidi ikilinganishwa na mwaka mzima wa kabla yake. Imesema hata watu ambao walikuwa wafungwa na kuachiwa huru sasa wamewekewa vizuizi na hawaruhusiwi kufanya safari nje ya nchi. Saudia

Wanasota katika jela za Saudi Arabia....

Tangu tarehe 21 Juni mwaka 2017 wakati Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia alimpomteua mwanaye, Muhammad, kuwa mrithi mpya wa kiti cha ufalme katika kile kilichotambuliwa kuwa ni mapinduzi baridi dhidi ya ndugu yake, nchi hiyo ilikumbwa na wimbi kubwa la ukatii, ukandamizaji na kunyongwa wapinzani na watetezi wa haki za kiraia. Hata hivyo jambo lililowashangaza zaidi wachambuzi wengi wa kimataifa si ukatili na unyama unaofanywa na utawala wa kifalme wa Saudia, kwa sababu hilo ni katika dhati na vinasaba vya utawala huo; bali ni kimya cha kushangaza cha jamii ya kimataifa na nchi za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu mbele ya ukatili na unyama huo. Vilevile jumuiya za kimataifa zinazodai kutetea haki za wanawake zimefyata mkia na kunyamaza kimya mbele ya ukatili na ukandamizaji mkubwa unaofanyika nchini Saudi Arabia dhidi ya wanaharakati wa kike ambao wengi wao wanasota na kupata sulubu za aina mbalimbali katika jela na korokoro za nchi hiyo. Ripoti ya Amnesty International inasema, wanaharakati wa kike wa kutetea haki za wanawake kama Loujain al-Hathloul, Nassima al-Sadah na Samar Badawi waliokuwa wameachiwa huru kutoka jela za Saudia mapema mwaka huu, sasa wamewekewa vizuizi vingi vinavyobana uhuru na harakati zao, na hiki ni kielelezo cha wazi cha ukiukaji wa uhuru wa kusema na kujieleza.  

Loujain al-Hathloul

Nchi hizo za Magharibi na taasisi zao eti kutetea haki za binadamu zimekhitari kunyamazia kimya ukatili huo unaofanyika Saudia Arabia lakini wakati huo huo zinashupalia na kuwakingia kifua wachochezi na wahalifu katika baadhi ya nchi kwa kisingizio cha kutetea haki za binadamu!

Kwa msingi huo swali linaloulizwa hapa ni kwamba, hadi lini jumuiya za kimataifa na nchi za Magharibi zitaendelea kufumbia macho na kunyamazia kimya ukatili wa baadhi ya madola yanayowakandamiza watetezi wa haki za binadamu na hata kuwachinja wengine kwa kutumia msumeno kwa sababu tu ya kupinga sera za utawala? Lini jumuiya na nchi hizo za Magharibi zitaacha kuuza uhai wa watetezi wa haki za binadamu na wapinzani wa serikali ya Saudia mkabala wa dola za mafuta za serikali ya Riyadh?   

Ni misimamo hii ya nchi za Magharibi ndiyo inayoushajiisha utawala kama wa Saudi Arabia kuwanyonga raia kwa sababu tu ya kubeba picha au bango lenye maandishi yanayopinga sera za utawala wa Riyadh. Ukweli huu unashuhudiwa katika ripoti ya Amnesty International ambayo inasema, mwezi uliopita Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia ilimnyonga kijana Muislamu wa madhehebu ya Shia, Mustafa bin Hashim bin Isa al-Darwish kwa tuhuma za kubeba bango lililokuwa na picha katika maandamano ya mwaka 2012.