Aug 07, 2021 11:28 UTC
  • Kikao cha Baraza la Usalama la UN kuhusu Afghanistan

Kikao maalumu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Afghanistan kilifanyika jana Ijumaa mjini New York.

Katika kikao hicho wanachama wa Baraza la Usalama ikiwemo Marekani, Uingereza, Russia, China na India wamelaani mashambulizi yanayolenga raia huko Afghanistan na wamesisitiza udharura wa kufanyika jitihada kubwa za kifikiwa mapatano ya kukomesha machafuko hayo. 

Mapigano makali yanayoendelea baina ya wapiganaji wa kundi la Taliban na jeshi la serikali kuu ya Afghanistan katika majimbo tofauti ya nchi hiyo na madai ya kundi hilo kwamba limedhibiti maeneo mengi ya Afghanistan ndiyo sababu kuu ya kuitishwa kikao maalumu cha jana cha Baraza la Usalama la UN. 

Baada ya kuanza kuondoka majeshi ya Marekani na jumuiya ya NATO katika ardhi ya Afghanistan ambako kulianza mwezi Mei kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa na serikali ya Joe Biden na kunatazamiwa kukamilika tarehe 31 mwezi Agosti badala ya Septemba 11 kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali, kundi la Taliban lilitumia fursa hiyo na kupanua udhibiti wake katika maeneo mengi ya Afghanistan na kuzidisha mashambulio dhidi ya vikosi vya serikali. 

Kwa sasa jamii ya kimataifa imepatwa na wasiwasi mkubwa kutokana na hali ya Afghanistan kwa kuzingatia kwamba, mapigano hayo yumkini yakazidisha mgogoro wa nchini hiyo ikiwa ni pamoja na hatari ya wimbi la wakimbizi kuelekea nchi jirani, kuzidisha umwagaji damu wa raia katika maeneo ya mapigano baina ya pande mbili, kuongezeka hatari ya harakati za makundi ya kigaidi kama al Qaida na Daesh, ongezeko la uzalishaji wa dawa za kulevya katika maeneo yanayodhibitiwa na Taliban na uwezekano wa kusambaratika serikali kuu ya Kabul. 

Wapiganaji wa Taliban

Inatupasa hapa kukiri kwamba, Marekani imehusika pakubwa katika kuibua hali mbaya ya sasa huko Aghanistan. Rais Joe Biden wa nchi hiyo tarehe 8 Julai alitoa amri ya kuondoka haraka na ghafla jeshi la Marekani huko Afghanistan ili kujikomboa katika kinamasi cha nchi hiyo. Wakati huo Biden alisema, umewadia wakati wa kukomesha vita virefu kuliko vyote vya Marekani.

Hadi sasa Marekani imeondoa asilimia 90 ya wanajeshi wake huko Afghanistan na kwa sababu hiyo kundi la Taliban limetumia fursa hiyo na kuteka maeneo mengi ya Afghanistan. Ilikuwa vigumu sana kwa serikali ya Kabul kuziba ombwe wa kiusalama uliosababishwa na kuondoka ghafla na bila ya uratibu wanajeshi wa Marekani na NATO huko Aghanistan.

Mtaalamu wa masuala ya Afghanistan, Ahmad Saidi anasema: “Marekani imewekeana mkataba wa kistratijia na serikali ya Afghanistan na vilevile makubaliano ya Doha na kundi la Taliban. Kwa msingi huo hakuna tofauti yoyote kwa Marekani kuhusu nani atadhibiti Afghanistan, kundi la Taliban, serikali ya Kabul au hata muungano wa pande zote mbili. Wamarekani wako tayari kushirikiana na pande zote mbili katika siku zijazo na wanasubiri kuona nani ataibuka mshindi katika machafuko ya sasa.”     

Hivi karibuni Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan alisema kuwa sababu ya machafuko ya sasa nchini humo ni uamuzi wa Marekani wa kuondoa ghafla majeshi yake nchini humo na ametahadharisha kuwa, hatua hiyo itakuwa na athari hasi. Hata hivyo Ghani amesisitiza kuwa, jeshi la Afghanistan lina uwezo na nguvu ya kuwarudisha nyuma na kuwashinda wapiganaji wa kundi la Taliban.  

Ashraf Ghani

Hata hivyo wataalamu wa mambo wanasema kuwa, uwezekano wa Afghanistan kutumbukia tena katika makucha ya Taliban umeongezeka sana hasa kwa kutilia maanani jinsi wapiganaji wa kundi hilo wanavyozidi kusonga mbele na kutokuwepo msaada wa kikosi cha anga kwa jeshi la serikali kuu ya nchi hiyo.  

Tags