Aug 17, 2021 02:33 UTC
  • Wanazuoni wa Kiislamu Bahrain wawakosoa watawala wa ukoo wa Aal Khalifa kwa kuvunjia heshima nembo za kidini

Wanazuoni wa Kiislamu wa Bahrain wamelaani vikali hatua za utawala wa kizazi cha Aal Khalifa wa nchi hiyo za kuvunjia heshima shughuli za kidini na nembo za maombolezo ya mwezi wa Muharram unaokumbusha mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) na kutoa wito wa kukomeshwa mara moja hatua hizo.

Taarifa iliyotolewa na wanazuoni wa Bahrain imesema kuwa, vizingiti vinavyowekwa na utawala wa Bahrain dhidi ya shughuli za Kiislamu za mwezi Muharram kwa kisingizio cha tahadhari za masuala ya afya haviwezi kutetewa kwa hoja za kimantiki, na kwamba hatua hizo ni siasa za kueneza chuki za kimadhehebu zinazolenga dini ya Uislamu kwa shabaha ya kuimarisha udhabiti wa kisiasa dhidi ya itikadi za kidini.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, shughuli za kidini za mwezi wa Muharram nchini Bahrain zinafanyika kwa kuchunga miongozo na maagizo yote ya wataalamu wa afya na kwa msingi huo hakuna haja ya kubinywa na kuwekewa vizuizi kila siku kwa kisingizio cha tahadhari za kiafya.

Taarifa ya wanazuoni wa Kiislamu nchini Bahrain imesema askari wa Bahrain wameendeleza mbinu za ukandamizaji za utawala wa Aal Khalifa kwa kukusanya bendera na mabango yote yenye nembo za kumbukumbu ya Muharram na mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika maeneo mengi ya nchi hiyo. 

Hatua hizo za utawala wa Bahrain zimepinga vikali na wananchi na makundi ya kidini nchini humo. 

Mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib aliuawa kikatili na utawala wa Bani Umayyah mwaka 61 Hijria katika mwezi huu wa Muharram.   

Tags