Aug 18, 2021 02:42 UTC
  • Kupiga marufuku utawala wa Bahrain maombolezo ya Imam Hussein (a.s); mwendelezo wa kunyanyaswa Waislamu wa Kishia

Kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, mwaka huu pia utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa nchini Bahrain umepiga marufuku kufanya shughuli zozote zile za Waislamu wa madhehebu ya Kishia za maombolezo ya Muharram na kumbukumbu ya kifo cha Imam Hussein (a.s).

Kwa akali asilimia 65 ya wananchi wa Bahrain ni Mashia. Licha ya kuwa Mashia ndio wanaounda asilimia kubwa ya wananchi wa Bahrain, lakini hawapati hata haki za watu walio wachache, na badala yake wamekuwa chini ya dhulma na ukandamizaji mkubwa tena wa kuratibiwa unaofanywa na utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Miongoni mwa haki za Mashia wa Bahrain zinazokanyangwa na utawala wa nchi hiyo ni haki za kimadhehebu. Ukweli ni kuwa, ubaguzi wa kimadhehebu ni sehemu ndogo tu ya mamia ya haki za Mashia zinazokiukwa na utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain.

Suala hilo hudhihirika zaidi unapowadia mwezi wa Muharram. Waislamu wa Kishia nchini Bahrain kama walivyo Mashia wengine ulimwenguni wanatambua kuwa, kufanya maombolezo ya Imam Hussein katika mwezi wa Muharram ni mambo ya kupewa kipaumbele ambayo haiwezekani kutoyafanya. Pamoja na hayo, utawal wa Aal Khalifa hauko tayari kuvumilia na kuwaacha Mashia wafanye marashimu hayo ya kimadhehebu. Kwa muktadha huo, kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, mwaka huu pia vyombo vya usalama vya Bahrain vimekwenda katika miji na mitaa mbalimbali ya nchi hiyo na kuendeleza mbinu za ukandamizaji za utawala wa Aal Khalifa kwa kukusanya bendera na mabango yote yenye nembo za kumbukumbu ya Muharram na mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika maeneo mengi ya nchi hiyo. 

 

Utawala wa Aal Khalifa umepiga marufuku na kuzuia maombolezo hayo katika hali ambayo, haki za kimadhehebu ni miongoni mwa haki zinazoungwa mkono na nyaraka mbalimbai za kimataifa za haki za binadamu. Katika kipengee cha pili cha tangazo la kimataifa la haki za binadamu lililopasishwa Disemba 10 mwaka 1948 inaelezwa kuwa: Kila mtu bila kujali rangi yake, kaumu, jinsia, lugha, dini, itikadi ya kisiasa au aina yoyote ile ya itikadi nyingine, utaifa, hali ya kijamii, utajiri na kadhalika ana haki ya kunufaika na haki zote na uhuru wote kwa mujibu wa tangazo hili.

Nukta muhimu ni hii kwamba, kipengee hiki cha Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu na sehemu nyingine za nyaraka na hati za kimataifa za haki za binadamu kinatilia mkazo kuhusiana na himaya ya haki za madhehebu ya waliowachache katika mataifa ya dunia, katika hali ambayo nchini Bahrain Mashia ni jamii ya waliowengi.

Jambo jingine ni kwamba, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Mashia nchini Bahrain umechukua wigo mpana zaidi zikitumiwa sababu mbalimbali kama ugonjwa wa Covid-19 na kuchunga miongozo ya afya. Hii ni katika hali ambayo, Bahrain sio tu kwamba, inafanya shughuli zingine kama mashindano ya michezo mbalimbali ndani ya nchi hiyo bali imekuwa mwenyeji wa hata mashindano ya Asia, yaliyojumuisha wanamichezo kutoka nchi mbalimbali.

Hivyo basi, corona ni kisingizio tu kinachotumiwa na utawala wa Bahrain kwa ajili ya kukandamiza na kuzuia shughuli za kimadhehebu za Waislamu wa Kishia. Katika uga huo, Maulamaa wa Bahrain wametoa taarifa wakisema kuwa, vizingiti vinavyowekwa na utawala wa Bahrain dhidi ya shughuli za Kiislamu za mwezi Muharram kwa kisingizio cha tahadhari za masuala ya afya haviwezi kutetewa kwa hoja za kimantiki, na kwamba hatua hizo ni siasa za kueneza chuki za kimadhehebu zinazolenga dini ya Uislamu kwa shabaha ya kuimarisha udhabiti wa kisiasa dhidi ya itikadi za kidini.

 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, shughuli za kidini za mwezi wa Muharram nchini Bahrain zinafanyika kwa kuchunga miongozo na maagizo yote ya wataalamu wa afya na kwa msingi huo hakuna haja ya kubinywa na kuwekewa vizuizi kila siku kwa kisingizio cha tahadhari za kiafya.

Ukandamizaji na unyanyasaji wa kidini wa utawala wa Aal Khalifa hususan dhidi ya Mashia wa nchi hiyo chimbuko lake ni sababu mbili. Sababu ya kwanza ni kuwa, utawala wa Aal Khalifa umeathirika na fikra za Uwahabi wa Saudi Arabia. Utawala wa Saudi Arabia kama ambavyo umekuwa ukiendesha siasa za ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Kishia ndani ya nchi hiyo, umekuwa pia ukiunga mkono unyanyasaji dhidi ya haki za Mashia nchini Bahrain.

Sababu ya pili ni kwamba, utawala wa Bahrain unatambua vyema kuwa, kupigania uhuru na kuunda utawala unaotokana na kura halisi za wananchi kabla ya yote chimbuko lake ni mafundisho ya kidini na vilevile fikra za viongozi wa dini wa Bahrain. Ni kwa msingi huo ndio maana utawala huo umepanua wigo wa ukandamizaji wa kimadhehebu. Miongoni mwa unyanyasaji na ukandamizaji huo ni kuzuia kufanyika maombolezo ya Muharram, kutia mbaroni watu, kuwashikilia kwa muda mrefu, kuwabaidisha viongozi wa kidini na wakati huo huo kuharibu nembo za kimadhehebu katika nchi hiyo ndogo ya Kiarabu.

Tags