Sep 01, 2021 07:21 UTC
  • Kambi ya kijeshi ya Marekani yashambuliwa kwa maroketi Deir ez-Zor

Duru za kiusalama zimeripoti habari ya kushambuliwa kwa maroketi kambi ya kijeshi ya Marekani katika mkoa wa Deir ez-Zor, mashariki mwa Syria.

Shirika la habari la al-Akhbariya limeripoti kuwa, kambi hiyo iliyoko katika eneo la Koniko lenye visima vya gesi viungani mwa mkoa huo ilivurumishiwa maroketi mawili usiku wa kuamkia leo.

Hakuna taarifa zozote rasmi zilizotolewa kuhusu maafa na hasara zilizosababishwa na shambulio hilo la jana usiku. Hiii si mara ya kwanza kwa kambi hiyo ya kijeshi ya Marekani kushambuliwa kwa maroketi. 

Kwa muda mrefu sasa, jeshi la Marekani na magenge ya kigaidi linayoyaunga mkono yamekalia kwa mabavu maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Syria kinyume cha sheria na bila ridhaa ya wananchi na serikali ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Kambi ya kijeshi ya US ikiteketea kwa moto mkoani Deir ez-Zor baada ya kushambuliwa

Kundi la uangalizi la Airwars, linalofuatilia operesheni za hujuma na mashambulio yanayofanywa na muungano wa kimataifa wa kijeshi unaoongozwa na Marekani wa eti kupambana na ISIS, lilitangaza hivi karibuni kuwa, tangu mwaka 2014 hadi sasa, maelfu ya raia wameuawa  katika mashambulio ya anga yaliyofanywa na muungano huo wa kijeshi katika nchi za Iraq na Syria.

Katika miaka ya karibuni, Marekani imelenga na kuua raia wasio na hatia katika nchi za Iraq na Syria kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi katika nchi hizo.

 

Tags