Sep 04, 2021 03:35 UTC
  • Wapalestina 45,000 wahudhuria Sala ya Ijumaa katika msikiti mtukufu wa Al Aqsa

Vyombo vya habari vya Palestina vimetangaza kuwa, Waislamu Wapalestina wamehudhuria kwa wingi katika Sala ya Ijumaa ya jana kwenye msikiti mtukufu wa Al Aqsa.

Idara ya Waqfu wa Kiislamu Baitul Muqaddas imetangaza kuwa, waumini 45,000 wamehudhuria Sala ya Ijumaa ya wiki hii katika msikiti wa Al Aqsa na Wapalestina wengine wengi wamezuiliwa kuingia msikitini humo.

Wiki hii pia kama ilivyokuwa katika wiki zilizopita, kabla ya kusaliwa Sala ya Ijumaa katika msikiti wa Al Aqsa, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel uliweka vizuizi vingi katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem), hususan katika eneo la kale la mji huo na lile la kandokando ya msikiti wa Al Aqsa.

Askari wa utawala haramu wa Israel walisambazwa kandokando ya msikiti wa Al Aqsa na kuweka vituo vya upekuzi ili kuwazuia vijana wa Kipalestina wasiingie msikitini humo.

Askari wa Kizayuni wakiweka vizuizi kuwazuia vijana wa Kipalestina wasiingie ndani ya msikiti wa Al Aqsa

Msikiti wa Al Aqsa umegeuzwa kuwa eneo la kutamba na kujifaragua askari wa utawala haramu wa Israel na walowezi wa Kizayuni wanaochukua hatua zinazolenga kuubadilisha utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa mji wa Quds (Jerusalem) na badala yake kuufanya kuwa na nembo za Uzayuni.

Utawala wa Kizayuni unachukua hatua hizo za kibeberu kuhusiana na mji wa Baitul Muqaddas na msikiti wa Al Aqsa wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO lilipitisha azimio mwaka 2016 lililopinga kuwepo uhusiano wowote wa kihistoria, kidini au kiutamaduni kati ya Mayahudi na maeneo matakatifu ya mji wa Quds na hasa msikiti wa Al Aqsa na kusisitiza kuwa, msikiti huo ni mahala patakatifu kwa Waislamu.

Mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) ulipo msikiti wa Al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu ni sehemu isiyotenganika na ardhi ya Palestina na moja ya maeneo matatu muhimu zaidi matakatifu ya Kiislamu.../

Tags