Sep 04, 2021 10:23 UTC
  • Wananchi wa Bahrain walaani kutumwa balozi wa Aal-Khalifa huko Israel

Wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano ya kulaani hatua ya utawala wa Aal-Khalifa ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, sanjari na pande mbili hizo kubadilishana mabalozi.

Katika maandamano hayo ya usiku wa kuamkia leo, wananchi wa Bahrain wamesema uamuzi huo wa Manama za kuanzisha uhusiano wa kawaida na Wazayuni unaenda kinyume na matakwa ya Wabahrain walio wengi.

Waandamanaji hao walisika wakipiga nara zinazosema "Kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ni uhaini" na "Tunapinga uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida."

Kadhalika waandamanaji hao wametangaza uungaji mkono wao kwa wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika mazingira ya kuogofya na vyombo vya usalama vya Aal-Khalifa, huku wakitaka waachiwe huru mara moja.

Wabahrain katika maandamano ya kuilaani Israel na kuonyesha uungaji mkono wao kwa Palestina

Alkhamizi ya juzi, Israel ilimteua Eitan Na’eh kuwa balozi wa kwanza wa utawala huo pandikizi nchini Bahrain, siku ambayo pia Khalid Yusuf Al-Jalahma, balozi wa kwanza wa Bahrain alikutana na Yair Lapid, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel katika bunge la utawala huo haramu (Knesset) na kukabidhi nakala za hati zake za utambulisho.

Miezi michache iliyopita, Bahrain ilitangaza rasmi kufungua ubalozi wake Tel Aviv baada ya pande hizo mbili kufikia mapatano ya kuanzisha uhusiano mwezi Septemba mwaka jana.

Katika dikrii ya Machi 30, Mfalme wa Bahrain Hamad Bin Isa Aal-Khalifa alitangaza kuanzisha ubalozi wa utawala huo wa kifalme huko Israel na akamteua Khalid Yusuf Al-Jalahma kuwa balozi wake.

 

Tags