Sep 05, 2021 03:16 UTC
  • Ukanda wa Gaza
    Ukanda wa Gaza

Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetishia kuwa, machaguo mengi yatakuwa mezani dhidi ya utawala ghasibu wa Israel iwapo utawala huo hautaondoa mzingiro wa pande zote dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza.

Daoud Shehab ambaye ni miongozi mwa viongozi wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina ameliambia shirika la habari la Uturuki kwamba, vivuko vya mpakani sasa vinatumiwa na Israel kama fimbo na silaha ya kulinyanyasa taifa la Palestina na kuzuia harakati za malalamiko na majibu ya Wapalestina dhidi ya dhulma za kila siku za utawala huo haramu.

Ameshiria miaka 15 ya mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kusema: Machaguo ya Wapalestina yataendelea kupanuka zaidi hadi pale utawala wa Kizayuni wa Israel utakapofuta mzingiro huo.

Daoud Shehab amesema ni haki ya taifa la Palestina kutumia nyenzo zote kwa ajili ya kupigania haki zake za kisiasa na kitaifa na kukabiliana na mbinu za utawala wa Kizayuni.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unalizingira eneo la Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006 wakati Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ilipoibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge la Palestina.

Tangu wakati huo Israel imekuwa ikizuia kuingizwa bidhaa zote muhimu katika eneo hilo kama vile chakula, dawa, vifaa vya ujenzi na kadhalika na kulifanya eneo hilo kukabiliwa na hali mbaya. 

Hivi sasa wakazi wa Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na mashaka na matatizo makubwa kwa ajili ya kupata huduma muhimu kama dawa, maji na chakula, huku asasi mbalimbali za kieneo na kimataifa zikitahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea maafa ya binadamu katika eneo hilo. 

Tags