Sep 06, 2021 03:03 UTC
  • Rais wa Israel na Mfalme wa Jordan wafanya mkutano wa siri

Rais wa utawala haramu wa Israel, Isaac Herzog amefichua kuwa alikutana na kufanya mazungumzo na Mfalme Abdullah II wa Jordan, mkutano wa siri uliofanyika wakati huu ambapo uhusiano wa Amman na Tel Aviv unazidi kuimarika.

Herzog amefichua hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali moja ya televisheni ya Kizayuni na kueleza kuwa: Wiki iliyopita, nilikutana na Mfalme wa Jordan katika kasri lake mjini Amman na tukafanya mazungumzo marefu.

Mahojiano hayo yalirushwa hewani jana Jumapili usiku, kuamkia mwaka mpya wa Kiyahudi unaoanza kuadhimishwa leo usiku. Habari zaidi zinasema kuwa, wawili hao walijadili msururu wa masuala ya kisiasa na kiuchumi, nishati, maji na kilimo.

Rais wa Israel ameeleza kuwa, "Jordan ni nchi muhimu sana, ninamuheshimu sana Mfalme Abdullah, kiongozi mkubwa na mwenye ushawishi mkubwa katika eneo." 

Julai mwaka huu pia, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vilitangaza kuwa, mfalme wa Jordan ameonana na Waziri Mkuu wa Israel, Naftali Benett katika mji mkuu Amman. Aidha mwezi Februari, Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan alikutana kwa siri na kificho na Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benny Gantz nchini Jordan.

Rais wa Israel, Isaac Herzog

Hii ni katika hali ambayo, Mfalme huyo wa Jordan mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuiunga mkono nchi huru ya Palestina ambayo mji wake mkuu utakuwa Quds Tukufu, sanjari na kuitaka jamii ya kimataifa iushinikize utawala huo ghasibu usitishe ujenzi wake wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina.

Akthari ya wananchi wa Jordan ambao asili yao ni Palestina hawaungi mkono uhusiano, ushirikiano na mkataba wa amani uliopo baina ya nchi yao na utawala wa Kizayuni.

Tags